ALIYEKUWA Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta, ameondolewa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi baada ya Serikali kugoma kumlipia kodi ya pango.
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania, mwanasiasa huyo mashuhuri, aliondolewa katika nyumba hiyo iliyopo Masaki, Dar es Salaam na kulazimika kuanza kuhamisha vyombo vyake tangu Ijumaa ya Julai 8, mwaka huu.
Kwa muda wote tangu akiwa Spika wa Bunge, Serikali ilikuwa inalipa kiasi cha dola 8,000 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh milioni 12 kwa ajili ya nyumba hiyo.
Sitta ambaye baadaye alikuwa waziri katika Wizara ya Afrika Mashariki pamoja na Uchukuzi, aliendelea kuishi katika nyumba hiyo kwa nafasi yake.
Kwa mujibu wa kijana aliyekuwa nyumbani hapo, alisema walianza kuhama tangu mwishoni mwa wiki iliyopita na wanaendelea kuhama kwa kuhamisha vitu kidogo kidogo.
“Ni kweli mzee amehama hapa, tangu Ijumaa tulikuwa tunahamisha vyombo taratibu na sijui kama Serikali imegoma kulipa kodi ama la, ila sasa amehamia jirani tu hapo Mtaa wa Manzese, hapa hapa Masaki.
“Nasikia nyumba imepata mpangaji mpya ndiyo maana wanahama,” alisema.
Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya, ili kuzungumzia hilo, alimtaka mwandishi kuwatafuta Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Wizara ya Fedha.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa utaratibu wa malipo kwa maspika wastaafu, ikiwa ni pamoja na matunzo na nyumba wanazoishi, Owen alisema Bunge halihusiki na stahiki zozote za wastaafu kwa mujibu wa sheria.
“Watafute Utumishi na Wizara ya Fedha, wao ndio wahusika, Ofisi ya Bunge haihusiki na stahiki zozote za wastaafu kwa mujibu wa sheria, isipokuwa Utumishi na Wizara ya Fedha ndio wahusika,” alisema.
Alipotafutwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema hana taarifa hizo za kuondolewa kwa Sitta hivyo atafuatilia.
Hata hivyo, alipotafutwa tena kupitia simu yake ya kiganjani, Kairuki alimtaka mwandishi kuwatafuta Hazina, kwamba ndio wanaoweza kulisemea jambo hilo.
“Naomba uwatafute Hazina wakupe ufafanuzi, halafu baadaye urudi kwangu,” alisema Kairuki.
Alipotafutwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kupitia simu yake ya kiganjani, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema: “Ufafanuzi kuhusu malipo kwa viongozi wastaafu unatolewa kwa viongozi husika na si kwa vyombo vya habari.”
Hali hiyo ya Sitta, imekuwa ni tofauti na aliyekuwa Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda, ambaye Serikali kupitia Bunge iligharimia matengenezo ya nyumba yake iliyoko Kijitonyama, Dar es Salaam, ambako ujenzi wake ulikumbana na lawama kali za wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo.
Spika Makinda alilaumiwa na majirani zake kwa kusababisha usumbufu baada ya kuziba njia inayopita katika eneo hilo kwenda maeneo ya Sinza.
Kwa mujibu wa Margaret Sitta ambaye ni mke wa Samweli Sitta na Mbunge wa Urambo, alisema kuwa walikuwa wakiishi kwenye nyumba hiyo ya Serikali kwa kuwa mumewe alikuwa Waziri wa Uchukuzi, lakini Baraza la Mawazili lilivunjwa tangu mwaka jana hivyo walipaswa kuhama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni