Jumatano, 20 Julai 2016
HIVI NDIVYO UNAVYOTAKIWA KUFANYA BAADA MIMBA KUTOKA
WASICHANA ambao walishika mimba na kuzitoa bila ya mtaalamu wa huduma za afya au wanawake walioshika mimba na zikatoka kwa bahati mbaya wote wanapaswa kupata huduma zitakazolinda afya zao pamoja na afya ya uzazi wao.
Vitu vya msingi katika kumhudumia msichana aliyetoa mimba ni pamoja na kumpeleka haraka katika kituo cha kutolea huduma za afya kinachotoa huduma za afya ya uzazi ambapo yataondolewa mabaki ya mimba na kusafishwa vizuri mfuko wake wa uzazi.
Wataalamu wanaoendesha kampeni ya 'Thamini Uhai, okoa maisha ya mama mjamzito na mtoto' inayoendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la World Lung Foundation Tanzania (WLF) chini ya ufadhili wa Swedish Internatinol Agency (SIDA), wanaushuri kuwa baada ya mgonjwa kusafishwa, atatibiwa matatizo yaliyojitokeza na kwamba atapewa ushauri nasaha ikiwa ni pamoja na kupewa dawa za uzazi wa mpango na kupangiwa tarehe ya kurudi endapo atapata matatizo mengine wakati kabla ya muda aliopangiwa kurudi haujafika hana budi kurudi upesi ili aweze kutatuliwa matatizo yake.
Huduma baada ya kutoa au mimba kuharibika zina umuhimu mkubwa sana ikiwa ni pamoja na kuzuia matatizo kwa mwanamke aliyetoa mimba mfano kutokwa na damu sana, pia mwanamke anaweza kupewa ushauri kuhusu afya ya uzazi na kuchagua njia ya uzazi wa mpango itakayomfaa vilevile atashauriwa kutofanya tendo la ndoa au ngono mpaka damu iache kabisa kutoka ukeni.
Iko wazi vijana ndio wanaongoza kwa kutoa mimba kwenye jamii zetu. Ila njia zifuatazo zinaweza kusaidia kuzuia kutoa mimba kwa vijana; kupiga punyeto, kushiriki michezo, kuacha ngono mpaka watakopoolewa, kujihusisha na shughuli za dini ambazo zinakataza ngono kabla au nje ya ndoa, kufanya shughuli nyingi za shule kama kujisomea,
kuepuka kutazama au kusoma habari zitakazoamsha hisia za ngono, kuhudhuria kliniki ya afya ya uzazi ili kupata elimu na ushauri utakaokufaa pamoja na njia za uzazi wa mpango na matumizi sahihi ya njia za uzazi wa mpango kutia ndani vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango na kondomu.
Kitengo maalumu cha Shirika la Afya Duniani (WHO) kinachoshughulikia nchi za Afrika mnamo Oktoba, 2000 kilikubaliana kuwa vijana wana haki ya kupata huduma za afya zitakazo wakinga na VVU pamoja na vitu vingine vitakavyohatarisha afya na ustawi wao kiujumla na huduma zinapaswa kuwa rafiki kwa vijana.
Kulingana na sera na muongozo wa uzazi wa mpango Tanzania, yeyote anayeweza kusababisha au kupata mimba anastahili kupata huduma za uzazi wa mpango. Na huduma hizi hutolewa bure kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali na baadhi ya vituo vya watu & mashirika binafsi bila malipo au kwa gharama nafuu.
Vijana waliobalehe wanapenda kupata huduma rafiki ya afya ya uzazi ikijumuisha kituo chenye mazingira rafiki kwa vijana ambapo vijana wanaweza kufika kwa urahisi, kituo chenye faragha na utunzaji wa siri za wateja, kituo chenye huduma zote stahiki kinachotoa huduma bure au kwa bei ndogo na nafuu na kituo chenye watumishi wenye heshima kwa wateja na wasio wepesi kuhukumu au kuwasema isivyofaa wateja.
Kuna njia nyingi za uzazi wa mpango ambazo zinamfaa kijana, njia hizi ni kuacha ngono, matumizi ya kondomu za kiume na za kike, vidonge vya uzazi wa mpango, sindano za uzazi wa mpango, vitanzi, vipandikizi, kumwaga nje shahawa (mbegu za kiume), kufunga uzazi na njia ya kunyonyesha.
Faida za uzazi wa mpango ni pamoja na kufanya mambo yafuatayo;
(i) Mwanamke hupata muda wa kutosha kupona kabisa baada ya kutoka mimba au kujifungua.
(ii) Mwanamke atapata muda wa kumtunza mtoto ikiwa alizaa mtoto na hakutoa mimba.
(iii) Hupunguza hatari ya kifo cha mwanamke kwa kuachanisha vizazi kwa angalau miaka miwili.
(iv) Mtoto atapata muda wa kutosha kunyonya ambako kutampa kinga ya mwili kuepuka magonjwa ya kuhara, humpa mtoto protini na nguvu pia husaidia ukuaji wa akili ya mtoto.
(v) Humpa mwanamke muda wa kufanya shughuli za kiuchumi zinazoingiza kipato kwa familia na taifa kiujumla.
(vi) Hupunguza hatari ya kusambaa kwa magonjwa ya njia ya ngono kama Kaswende na VVU, mfano njia ya uzazi wa mpango zinazohusisha aina zote za kondomu.
(vii) Huzuia aina fulani za vivimbe katika viungo vya uzazi vya mwanamke hasa njia za uzazi wa mpango zenye homoni ya istrojeni.
(viii) Hupunguza hatari ya Saratani ya Matiti, Saratani za Ovari na mfuko wa kizazi hasa njia za uzazi wa mpango zenye homoni.
(ix) Hutoa nafasi ya kuchunguzwa na kugundulika kwa magonjwa mapema. Mfano ukiwa unawekewa Kitanzi lazima uke uchunguzwe vizuri kabla ya kuwekewa.
(x) Dawa za uzazi wa mpango zinaweza kutumika kutibu matatizo ya kutokwa na damu ukeni kwa wingi kitaalamu hujulikana kama Dysfunction Uterine Bleeding.
(xi) Hupunguza upoteaji wa damu kipindi cha hedhi pale unapotumia njia za uzazi wa mpango zenye homoni.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni