Jumamosi, 16 Julai 2016
MAKINDA ANG'ATA WAKURUGENZI NHIF
Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambayo Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda ni Mwenyekiti wake, imewatumbua wakurugenzi 9 wa mfuko huo kutokana na ufujaji wa mabilioni ya fedha za umma uliobainika.
Uamuzi huo umeripotiwa kuwa umetokana na usimamizi wao mbovu uliopelekea Mfuko kupata hasara ya shilingi bilioni 3.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na gazeti moja la kila siku, baadhi ya waliosimamishwa kazi na Bodi ya NHIF na idara walizokuwa wanazimamia kwenye mabado ni Grace Lekule (Utawala), Raphael Mwamwoto (Uendeshaji), Frank Lekela (Udhibiti Ubora wa Huduma) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Michael Mhando.
Panga hilo pia limewapitia Yujin Mikongoti (Mifuko ya Afya ya Jamii), Ally Othman (Tehama), Rehani Athuman (Tafiti na Masoko), Makala (Sheria) na Jackson Burula (Manunuzi).
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kuwa anafahamu kuwepo kwa mtikisiko huo na kwamba majukumu yote alimwachia Mwenyekiti wa Bodi, Anne Makinda.
“Nipo Muleba, ila majukumu yote tayari niliyaacha kwa Bodi ya Mama Makinda. Yeye atakuwa anajua kila kitu,” Waziri Mwalimu ananukuliwa.
Taarifa hii imekuja ikiwa ni miezi michache imepita tangu Mhasibu wa NHIF mkoa wa Mara, Francis Mchati kusimamishwa kazi akihusishwa na upotevu wa shilingi bilioni 3.
Mtuhumiwa alikabidhiwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambayo inaendelea na uchunguzi kwa hatua nyingine za kisheria.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni