Jumanne, 19 Julai 2016

HII NDIO SABABU YA DAGAA WA KIGOMA KUUZWA BEI GHARI



KAMA ukibahatika kutembelea katika masoko mbalimbali nchini bei ya Dagaa Ndagala maarufu kama Dagaa wa Kigoma mara nyingi imekuwa juu ikilinganishwa na dagaa wengine.

Dagaa hao ambao wanapatikana katika Ziwa Tanganyika wanapendwa na watu wengi na sifa kubwa ya kitoweo hicho ni kutokuwa na mchanga.

Kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma, wengi wanaendesha maisha yao kutokana na kuuza kitoweo hicho ambacho kimekuwa kikisafirishwa na kuuzwa katika maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani kama za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Vijiji vya Ibirizi, Mwamgongo, Nkonkwa, Lagosa na Katumbi ambavyo viko katika mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma ni maarufu kwa kufanya biashara hiyo ya dagaa.

Katika vijiji hicho makundi ya wanawake na vijana wamejiajiri katika biashara hiyo na wengi wanakiri kwamba imewasaidia kuendesha maisha yao na familia zao.

Gazeti hili lilizungumza na wafanyabiashara na wavuvi ili kujua siri ya mafanikio hayo.

Mmoja wa wafanyabiashara hao kutoka Kijiji cha Katumbi, Salama Athumani, anasema dagaa hao huandaliwa katika mazingira masafi na kuwafanya kuwa bora zaidi.

“Ni nadra mtu kula dagaa wa Kigoma halafu wawe na mchanga na kama ikitokea ni mara chache labda mtu aliokota waliodondoka chini na kuchanganya na wengine,” anasema Salama.

UKAUSHAJI

Kwa kiasi kikubwa samaki wadogo (dagaa) huuzwa wakiwa tayari wamekaushwa lakini jamii nyingi za wavuvi awali zilikuwa zikitumia mbinu ambazo hazikuwa salama kiafya ambazo zilichangia kupunguza ubora wa kitoweo hicho kutokana na kuharibika pamoja na upotevu wa samaki.

Katika maeneo ya Afrika inakadiriwa kuwa samaki wanaoharibika kabla ya kumfikia mlaji ni kati ya asilimia 20 hadi 25 na wakati mwingine hufikia asilimia 50.

Ofisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, John Mapunda, anasema kutokana na ongezeko la watu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, mahitaji ya samaki yameendelea kuongezeka siku hadi siku, hivyo kusababisha uzalishaji samaki kutoka kwenye vyanzo vya asili kupungua kwa kasi.

TEKNOLOJIA YA KICHANJA

Shirika la Chakula Duniani (FAO), lilitoa Waraka wa Kuzingatiwa wa Uvuvi Endelevu (Code of Conduct for Responsible Fisheries) unaosisitiza umuhimu wa kupunguza upotevu wa samaki.

Pamoja na waraka huo Shirika hilo lilikuwa linatekeleza mradi katika jamii za wavuvi wa samaki ndogondogo zilizoko katika Ziwa Tanganyika, nchini Burundi.

Mradi huo ulijikita katika kuleta mbinu za gharama nafuu za ukaushaji dagaa kwa kuanika kwenye kichanja ili kuhakikisha kitoweo hicho kinakuwa salama na kuwa na soko zuri.

Mbinu ambayo imeonekana kuwa na manufaa makubwa hivi sasa imesambaa hadi katika vijiji vilivyoko mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.

Patiasi Deo ambaye ni mfanyabiashara katika Kijiji cha Lagosa, anasema ubora wa kitoweo hicho unatokana na uandaaji wake aliodai kuwa ni wa kimataifa.

“Walikuja watu wakatufundisha kukausha dagaa kwa kuwaweka katika vichanja badala ya kuanika chini. Zamani tulikuwa tunaanika chini halafu wakikauka tunawachekecha lakini mchanga ulikuwa hautoki wote.

“Yaani ukianika chini mchanga, mvua na matope huharibu matokeo yake unaweza kujiharibia soko kwa sababu mtu akinunua akakuta wana mchanga anaweza asirudi tena kwako,” anasema Joseph.

Mfanyabiashara mwingine kutoka katika Kijiji cha Mwamgongo, Ismail Juma, anasema ukaushaji dagaa kwa kutumia vichanja umeimarisha usafi na usalama wa dagaa hao.

“Tangu tuanze kukausha dagaa kwenye vichanja bei imepanda na imekuwa ni faraja kwetu wafanyabiashara na wavuvi,” anasema Juma.

Juma anasema huwa wananunua dagaa wabichi kwa Sh 12,000 kwa karai moja ambapo baada ya kukaushwa hupatikana kilo tano. Katika eneo hilo kilo moja huuzwa kati ya Sh 8,000 hadi 10,000 kutegemeana na msimu.

Kwasasa bei ya Dagaa Kigoma katika masoko ya jijini Dar es Salaam ni kati ya Sh 23,000 hadi 25,000.

“Kwasasa dagaa wanapatikana kwa wingi kwa sababu huu ni msimu wake, lakini kuna wakati wanakuwa wachache kwahiyo lazima bei itakuwa juu tu,” anasema.

Ripoti ya FAO iliyotolewa mwaka juzi inayoonyesha kuridhishwa na mradi huo kwani pia umesaidia kutunza rasilimali za ziwa Tanganyika.

Ofisa wa FAO Yvette Diei Ouadi, anasema waliwasaidia wavuvi kutengeneza chanja za kukausha zilizo juu kidogo na zenye kifuniko ili kuzuia mvua na kwamba baada ya muda mfupi vijiji vingine vilianza kuiga mbinu hiyo.

Kabla ya kuja mbinu hiyo asilimia 15 ya samaki waliokamatwa walikuwa wanapotea au wanaharibika wakati wa kukaushwa.

COSTECH, TAFIRI

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI), hivi sasa wanatekeleza mradi unaolenga kutumia teknolojia nafuu na rafiki wa mazingira katika ukaushaji wa samaki katika vijiji vilivyoko mwambao wa Ziwa Nyasa.

Wastani wa tani 30,000 huvuliwa kwa mwaka kutoka Ziwa Nyasa huku upotevu wa samaki hasa wakati wa mvua hukifikia hadi asilimia 50 ya samaki waliovuliwa na hasa kwa samaki wadogo. Upotevu hutokana na desturi za ukaushaji samaki kwa kutumia moshi au kwa kuanika mchangani.

TAFIRI kwa msaada wa fedha kutoka COSTECH imeboresha makaushio ya gharama nafuu yanayotumia nishati ya jua kwa ajili ya ukaushaji wa samaki wadogo wadogo.

Mradi huo ulianza mwaka 2013 ukiwa na lengo la kuboresha mbinu za matumizi ya nishati ya jua katika kukausha samaki kwa kutumia makaushio au majiko yanayotumia nishati ya jua.

Majiko hayo yanatumia vifaa vinavyopatikana kirahisi katika mazingira husika. Yapo makaushio ya hema, boksi, shimo na meza ya wazi ambayo hufanya kazi kwa kuzingatia uwezo wa kuhifadhi joto na unyevu nje na ndani, mwendo kasi wa upepo wa nje, kasi ya ukaushaji na muda wa bidhaa kudumu bila kuharibika baada ya kukaushwa.

Sampuli za samaki wakavu waliochakatwa zilipelekwa kwenye maabara za Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) ili kuchunguza viinilishe na madini na aina ya kaushio la hema limeonyesha kufanya vizuri zaidi ikilinganishwa na makaushio mengine.

FAIDA ZA DAGAA

Dk. Willy Sangu kutoka Manispaa ya Ilala, anasema dagaa ni chanzo cha madini ya chuma mwilini. “Ni chakula bora kwetu sote ambacho kinaweza kuliwa na wali, ugali, ndizi za kuchemsha, mihogo, viazi na vyakula vingine.”

Kwa ujumla teknolojia hiyo ya ukaushaji dagaa ni nafuu na imechangia ubora wa kitoweo hicho kuongezeka siku hadi siku na kuboresha kipato cha wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara ya samaki katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, hivyo ni muhimu ikaendelezwa katika maeneo mengine.

Maoni 4 :

  1. Natamani sana kuifanya hii biashara ila sina uzoefu 😌🤔🤔🤔

    JibuFuta
  2. Mimi naitaji nifahamu masoko yalipo maana ninao dagaa wa kigoma.

    JibuFuta
  3. 0744624885 nichek Boss

    JibuFuta