Jumatano, 13 Julai 2016
ANAYEDAIWA KUHAMISHA SHILINGI MILIONI SABA KWA DAKIKA AFIKISHWA MAHAKAMANI
Mfanyabiashara Mohamed Mustapha (anayeongea na simu) na wenzake, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana kukabiliana na tuhuma za kuibia Serikali kodi ya Sh milioni 7 kwa kila dakika kwa kipindi kirefu.
**
Hatimaye mfanyabiashara aliyetajwa na Rais John Magufuli kuwa amekuwa akiibia Serikali takriban Sh7 milioni kwa dakika, amepandishwa kizimbani na wenzake wanne na kusomewa mashtaka 199, wote kwa pamoja.
Mfanyabiashara huyo, Mohamed Mustafa Yusufali na wenzake Alloyscious Gonzaga Mandago, Isaac Wilfred Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Seif Kabla, walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh15 bilioni.
Katika ya mashtaka hayo, Yusufali maarufu kwa majina ya Mohamedali, Choma au Jamalii anakabiliwa na mashtaka 198 yeye peke yake huku wenzake wakikabiliwa shtaka moja la utakatishaji fedha.
Kutokana na wingi wa mashtaka hayo, waendesha mashtaka wawili; Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai walilazimika kubadilishana ili kuwapa muda wa kupumua.
Kutokana na kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na shtaka la kutakatisha fedha, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu na kulingana na mashtaka yanayowakabili, hayana dhamana.
Baada ya kumaliza kuwasomewa mashtaka hayo, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Hivyo, Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi anayesikiliza kesi hiyo aliamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu hadi Julai 25, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Kabla ya kupandishwa kizimbani, Yusufali alitajwa na Rais Magufuli kuwa ana mashine inayotoa risiti za kielektroniki (EFD) nje ya mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuzisambaza kwa wafanyabiashara wengine, hivyo kujiingizia Sh7 milioni kwa dakika.
Rais Magufuli alieleza kuwa mtandao wake unawashirikisha watumishi wa TRA na Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela), hivyo kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
Katika mashtaka hayo, Yusufali anakabiliwa na mashtaka 181 ya kughushi, mashtaka 15 ya kuwasilisha nyaraka za uongo, udanganyifu katika kulipa kodi moja, shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh15,645,944,361, huku shtaka moja tu la utakatishaji fedha ndilo likimhusisha na wenzake.
Waendesha mashtaka hao walidai kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akighushi nyaraka za kampuni mbalimbali, kuonyesha kuwa zimesajiliwa na zinaendesha shughuli zake nchini kihalali wakati akijua siyo kweli.
Pia, walidai kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akiwasilisha nyaraka za uongo TRA.
Kuhusu shtaka la kutakatisha fedha, upande wa mashtaka ulidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja kati ya Machi 2011 na Januari 2016, walitakatisha Sh1,895,88500 kwa kujifanya kuwa ni malipo ya mikopo waliyoipokea kwa watu mbalimbali.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa kati ya Januari 2008 na Januari 2016, mfanyabiashara huyo alifanya udanganyifu katika kuwasilisha kwa Kamishna Mkuu wa TRA taarifa ya uongo ya marejesho ya mapato, hivyo kuikosesha Serikali mapato ya kodi ya VAT zaidi ya Sh15.6 bilioni.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni