Jumatano, 20 Julai 2016

NYAYO ZA LOWASA KUITIKISA CCM DODOMA



Wakati CCM ikijiandaa kumkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti, suala la masalia ya Edward Lowassa linaweza kuchukua nafasi kubwa katika vikao vitatu vya juu vinavyofanyika kwa mara ya kwanza tangu kumalizika Uchaguzi Mkuu mwaka jana.

Ni dhahiri kuwa Mkutano Mkuu Maalumu ulio na ajenda moja tu ya kumchagua mwenyekiti mpya hautakuwa na nafasi ya kujadili ajenda nyingine, lakini Halmashauri Kuu iliyogawanyika baada ya Lowassa kuenguliwa kwenye mbio za urais, inaweza kuchukua muda kujadili CCM mpya baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kujiondoa Julai 28 mwaka jana.

CCM itaanzia mikutano yake kwa kikao cha Kamati Kuu, ambayo hufanya maandalizi ya kikao cha Halmashauri Kuu kitakachofanyika Ijumaa na kumalizia na Mkutano Mkuu Jumamosi wiki hii.

Pia kutakuwa na kikao kingine cha Halmashauri Kuu kitakachofanyika Jumapili ambacho kwa sehemu kubwa kinatarajiwa kujadili taarifa za wasaliti zilizoandaliwa na kamati za siasa za mikoa na huenda kikatoa maamuzi mazito yanayobeba mustakbali wa kuijenga “CCM ya Magufuli”.

Lakini makada wengi waliohojiwa  kuhusu suala la masalia ya Lowassa kuibuka kwenye vikao hivyo, walipinga wakisema waliomuunga mkono mwanasiasa huyo maarufu, walifanya hivyo wakati akiwa CCM na kwa kuwa hawakumfuata hawatarajii suala hilo kuibuka tena.

“Makundi ndani ya CCM yalikwisha baada ya Magufuli kupitishwa kukabidhiwa kijiti,” alisema mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Geita na mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku Msukuma alipoulizwa kuhusu suala la Lowassa kuibuka kwenye vikao hivyo vya juu.

Msukuma, ambaye alifanya mbwembwe za kuhama kambi ya Bernard Membe kwa kutua na helikopta kwenye mkutano wa Lowassa mjini Arusha, alisema wakati CCM ikisaka mgombea wake wa urais, kulikuwa na makundi zaidi ya 40.

“Wakati ule kila mgombea alikuwa na kundi. Ila kwa sasa sidhani kama hali hiyo bado ipo maana baada ya mgombea kupatikana kila mmoja alimuunga mkono,” alisema Msukuma.

Kauli kama hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida ambaye alisema kila mwenyekiti huja na timu yake, hivyo kama kutakuwa na mageuzi, si kitu kinachohitaji mjadala.

“(Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin) Mkapa alipomuachia uenyekiti (Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya) Kikwete alikuja na timu yake mpya. Kama utakumbuka katibu mkuu wake alikuwa Yusuf Makamba,” alisema Madabida ambaye naye alikuwa miongoni mwa wenyeviti waliomuunga mkono Lowassa.

“Nina matarajio na rais. Naamini atakifanya chama kuwa imara zaidi na kuleta mageuzi ya kisiasa na kiuchumi. Mabadiliko ni kawaida na wenyeviti wapya huja na kamati kuu na sekretarieti mpya.”

Hata hivyo, kuanzia Januari mwaka huu kamati za siasa za mikoa zimekuwa zikikutana kujadili watu wanaoitwa ni wasaliti na kupeleka mapendekezo ya hatua dhidi yao kwenye vikao vya juu.

Rais Magufuli, ambaye hajawahi kushika uongozi wa chama, anaaminika kuwa ataifanya CCM kuwa na sura, mwelekeo na ushawishi mpya, hali itakayochangia kukata mizizi iliyojengwa na wanasiasa mashuhuri.

Kutokana na hali ilivyokuwa wakati Lowassa akiondoka CCM na mtikisiko aliouacha, chama hicho hakitaweza kujipapatua bila kumtaja Lowassa na mtandao wake wakati kikijadili jinsi ya kusonga mbele.

Mbunge huyo wa zamani wa Monduli amekuwa akijadiliwa kwa ushabiki mkubwa ndani na nje ya vikao halali vya CCM tangu alipojitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 1995 kuwania urais akiwa na umri wa miaka 42.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, mwanasiasa huyo aliwagawa makada wa CCM na alipohamia Chadema kuna kundi lilimfuata na jingine kubakia, huku baadhi ya wanachama kwenye kundi hilo wakituhumiwa kwa usaliti.

Baada ya kujiondoa CCM Julai 28, 2015 na kujiunga Chadema alikoteuliwa kuwa mgombea urais na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), mashambulizi mengi kutoka CCM yalielekezwa kwake.

Vikao vinavyosubiriwa kutia muhuri mapendekezo ya kamati za siasa za mikoa ndivyo vinavyofanyika wiki hii mjini Dodoma baada ya CCM kuitisha mkutano mkuu maalumu ili kukamilisha taratibu za kumkabidhi Rais Magufuli usukani wa chama hicho.

 Halmashauri Kuu ya JPM
Halmashauri Kuu ya JPM inatarajiwa kutumbua watendaji wazembe, goigoi, wasiokwenda na kasi yake, wabadhirifu wa fedha za chama na wengine ambao uwapo wao ni mzigo kwa CCM.

Hivyo, Halmashauri Kuu itasuka upya chama, pia kwa kujaza nafasi za watendaji waliojiuzulu kutokana na desturi ya chama hicho.

Kwa kawaida, CCM inapopata mwenyekiti mpya, sekretarieti yote hujiuzulu ili kumpa nafasi kiongozi huyo kupanga safu yake, alisema msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka juzi alipoongea na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Sekretarieti inaongozwa na katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye anaaminika kuwa alifanya kazi kubwa ya kukirudishia chama hicho nguvu wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita ambao ulikuwa na ushindani mkubwa.

Wengine ni Vuai Ali Vuai (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), Rajab Luhavi (Naibu Katibu Mkuu Bara), Mohamed Seif Khatib (Katibu wa Oganaizesheni) na Nape Nnauye (Katibu wa Itikadi na Uenezi).

Wengine ni Dk Asha-Rose Migiro (Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje), na Zakia Meghji (Katibu wa Uchumi na Fedha).

Halmashauri Kuu ya JPM inatarajiwa pia kujadili hali ya hewa ya kisiasa ndani ya chama, kupanga mikakati ya kuimarisha uchumi na kutekeleza mapendekezo ya kuwafukuza wasaliti, ambao wanatuhumiwa kuwa waliendelea kumuunga mkono Lowassa wakati wa kampeni na kusababisha chama kupoteza baadhi ya majimbo.

 Oktoba 30, 2015 baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi wa urais na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva iliandaliwa hafla fupi makao makuu ya CCM Lumumba, ambako Dk Magufuli alimwambia mwenyekiti wake akisema: “Umezungukwa na wanafiki na watu ambao ulidhani watakusaidia kwenye chama, lakini wamekuangusha”

Miongoni mwa watu ambao hata wakati wa kampeni alikuwa anawashutumu ni waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini, lakini wakahamia upinzani na kuibeza Serikali.

 Dk Magufuli anaonekana alikuwa anawalenga Lowassa na mwenzake Frederick Sumaye ambao waliunda safu kabambe ndani ya Chadema kuisakama CCM.

Orodha ya watakaotumbuliwa na NEC ya JPM ni ndefu. Baadhi yao ni makada waliojitokeza hadharani kupinga utaratibu uliotumiwa na wazee kukata jina la Lowassa kugombea urais.

Hata baada ya CCM kumteua Dk Magufuli kuwa mgombea urais, bado wapo waliompinga wakidai hana mizizi katika chama.

Wengine wanaoweza kutumbuliwa ni walioanzisha wimbo wa “Tuna imani na Lowassa” ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM wakionyesha utiifu wao kwa Lowassa badala ya Mwenyekiti Kikwete aliyeongoza kikao cha Kamati Kuu kilichotoa majina matano ya waliopitishwa kugombea urais bila ya jina la Lowassa kuwamo.

Wengine wanaoweza kutupiwa virago ni makada waliosusa kumpigia debe Dk Magufuli pamoja na waliodaiwa kukitelekeza chama.

Habari nyingine zinasema waliopendekezwa kufukuzwa na vikao vya wilayani ni wanaodaiwa kubadilika usiku na kusaidia Ukawa, wakiwamo wenyeviti wa mikoa na makatibu.

Pia, wamo baadhi ya wabunge na wafanyabiashara waliokuwa wanawabeba mamia kwa makumi ya wanachama kwenda nyumbani kwa Lowassa mjini Dodoma kuonyesha kumuunga mkono

HIVI NDIVYO UNAVYOTAKIWA KUFANYA BAADA MIMBA KUTOKA



WASICHANA ambao walishika mimba na kuzitoa bila ya mtaalamu wa huduma za afya au wanawake walioshika mimba na zikatoka kwa bahati mbaya wote wanapaswa kupata huduma zitakazolinda afya zao pamoja na afya ya uzazi wao.

Vitu vya msingi katika kumhudumia msichana aliyetoa mimba ni pamoja na kumpeleka haraka katika kituo cha kutolea huduma za afya kinachotoa huduma za afya ya uzazi ambapo yataondolewa mabaki ya mimba na kusafishwa vizuri mfuko wake wa uzazi.

Wataalamu wanaoendesha kampeni ya 'Thamini Uhai, okoa maisha ya mama mjamzito na mtoto' inayoendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la World Lung Foundation Tanzania (WLF) chini ya ufadhili wa Swedish Internatinol Agency (SIDA), wanaushuri kuwa baada ya mgonjwa kusafishwa, atatibiwa matatizo yaliyojitokeza na kwamba atapewa ushauri nasaha ikiwa ni pamoja na kupewa dawa za uzazi wa mpango na kupangiwa tarehe ya kurudi endapo atapata matatizo mengine wakati kabla ya muda aliopangiwa kurudi haujafika hana budi kurudi upesi ili aweze kutatuliwa matatizo yake.

Huduma baada ya kutoa au mimba kuharibika zina umuhimu mkubwa sana ikiwa ni pamoja na kuzuia matatizo kwa mwanamke aliyetoa mimba mfano kutokwa na damu sana, pia mwanamke anaweza kupewa  ushauri kuhusu afya ya uzazi na kuchagua njia ya uzazi wa mpango itakayomfaa vilevile atashauriwa kutofanya tendo la ndoa au ngono mpaka damu iache kabisa kutoka ukeni.

Iko wazi vijana ndio wanaongoza kwa kutoa mimba kwenye jamii zetu. Ila njia zifuatazo zinaweza kusaidia kuzuia kutoa mimba kwa vijana; kupiga punyeto, kushiriki michezo, kuacha ngono mpaka watakopoolewa, kujihusisha na shughuli za dini ambazo zinakataza ngono kabla au nje ya ndoa, kufanya shughuli nyingi za shule kama kujisomea,

kuepuka kutazama au kusoma habari zitakazoamsha hisia za ngono, kuhudhuria kliniki ya afya ya uzazi ili kupata elimu na ushauri utakaokufaa pamoja na njia za uzazi wa mpango na matumizi sahihi ya njia za uzazi wa mpango kutia ndani vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango na kondomu.

Kitengo maalumu cha Shirika la Afya Duniani (WHO) kinachoshughulikia nchi za Afrika mnamo Oktoba, 2000 kilikubaliana kuwa vijana wana haki ya kupata huduma za afya zitakazo wakinga na VVU pamoja na vitu vingine vitakavyohatarisha afya na ustawi wao kiujumla na huduma zinapaswa kuwa rafiki kwa vijana.

Kulingana na sera na muongozo wa uzazi wa mpango Tanzania, yeyote anayeweza kusababisha au kupata mimba anastahili kupata huduma za uzazi wa mpango. Na huduma hizi hutolewa bure kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali na baadhi ya vituo vya watu & mashirika binafsi bila malipo au kwa gharama nafuu.

Vijana waliobalehe wanapenda kupata huduma rafiki ya afya ya uzazi ikijumuisha kituo chenye mazingira rafiki kwa vijana ambapo vijana wanaweza kufika kwa urahisi, kituo chenye faragha na utunzaji wa siri za wateja, kituo chenye huduma zote stahiki kinachotoa huduma bure au kwa bei ndogo na nafuu na kituo chenye watumishi wenye heshima kwa wateja na wasio wepesi kuhukumu au kuwasema isivyofaa wateja.

Kuna njia nyingi za uzazi wa mpango ambazo zinamfaa kijana, njia hizi ni kuacha ngono, matumizi ya kondomu za kiume na za kike, vidonge vya uzazi wa mpango, sindano za uzazi wa mpango, vitanzi, vipandikizi, kumwaga nje shahawa (mbegu za kiume), kufunga uzazi na njia ya kunyonyesha.

Faida za uzazi wa mpango ni pamoja na kufanya mambo yafuatayo;

(i) Mwanamke hupata muda wa kutosha kupona kabisa baada ya kutoka mimba au kujifungua.

(ii) Mwanamke atapata muda wa kumtunza mtoto ikiwa alizaa mtoto na hakutoa mimba.

(iii) Hupunguza hatari ya kifo cha mwanamke kwa kuachanisha vizazi kwa angalau miaka miwili.

(iv) Mtoto atapata muda wa kutosha kunyonya ambako kutampa kinga ya mwili kuepuka magonjwa ya kuhara, humpa mtoto protini na nguvu pia husaidia ukuaji wa akili ya mtoto.

(v) Humpa mwanamke muda wa kufanya shughuli za kiuchumi zinazoingiza kipato kwa familia na taifa kiujumla.

(vi) Hupunguza hatari ya kusambaa kwa magonjwa ya njia ya ngono kama Kaswende na VVU, mfano njia ya uzazi wa mpango zinazohusisha aina zote za kondomu.

(vii) Huzuia aina fulani za vivimbe katika viungo vya uzazi vya mwanamke hasa njia za uzazi wa mpango zenye homoni ya istrojeni.

(viii) Hupunguza hatari ya Saratani ya Matiti, Saratani za Ovari na mfuko wa kizazi hasa njia za uzazi wa mpango zenye homoni.

(ix) Hutoa nafasi ya kuchunguzwa na kugundulika kwa magonjwa mapema. Mfano ukiwa unawekewa Kitanzi lazima uke uchunguzwe vizuri kabla ya kuwekewa.

(x) Dawa za uzazi wa mpango zinaweza kutumika kutibu matatizo ya kutokwa na damu ukeni kwa wingi kitaalamu hujulikana kama Dysfunction Uterine Bleeding.

(xi) Hupunguza upoteaji wa damu kipindi cha hedhi pale unapotumia njia za uzazi wa mpango zenye homoni.

🤓 KUFANIKIWA KATIKA MAISHA SIO ELIMU BALI UJASIRI,KUJIAMINI NA KUTHUBUT




🕵 Ukichunguza katika jamii, utabaini kuwa sehemu kubwa ya matajiri ni wale ambao wana elimu ndogo ama hawakusoma kabisa.
Katika miji na maeneo yote; wenye majengo ya maana, wenye makampuni makubwa, wenye utitiri wa malori na mabasi, wenye maduka makubwa ni wale wa "darasa la saba” au wale ambao hawakuingia darasani kabisa.

Wasomi wengi wana maisha ya kawaida yaani yale ya kiwango cha kubadilisha mboga, wakijitahidi sana wanaishia kujenga nyumba za kuishi  na  magari mawili ya kutembelea (tena kwa mikopo!).

Wapo wasomi wengi tu wanaoishi kimasikini, kwa lugha ya kistaarabu tunasema wana maisha ya kuungaunga. Kiukweli idadi ya wasomi walio matajiri ni ndogo sana.

Lakini Umasikini wa wasomi wengi umeanzia huko shuleni na vyuoni wanakopatia usomi wao. Madarasani kuna mambo mawili wanafundishwa wasomi ambayo ndio yanayowaroga.

Hii inachangiwa na mambo mawili.

1⃣ Wameelimishwa na kuaminishwa kwamba yule anaepata maswali yote kwa usahihi ndio anaonekana amefaulu. Ukikosea unahesabika kuwa u mjinga na wenyewe wanaita umefeli.
Hata hivyo katika maisha ya kawaida hasa kwenye mchakato wa kutafuta hela, kujaribu na kukosea ni sehemu ya mafanikio.
Kadiri unavyojaribu na kukosea mara nyingi ndivyo unavyojifunza na ndivyo nafasi ya kutajirika kwako inakuwa kubwa!
Wasomi wengi kwa sababu ya "mentality" ya kuogopa kukosea huwa hawapendi kujaribu biashara kwa hofu ya kushindwa kuiendesha, na huamua kufa kimasikini wakitegemea mishahara pekee kwa sababu mishahara ndio pato lao la uhakika.

2⃣ Madarasani kunahimizwa ubinafsi badala ya umoja. Angalia namna mitihani inavyofanyika. Kila mwanafunzi anafanya mtihani peke yake, na ukikutwa unaangalizia ama mnasaidiana na mwenzio ndani ya chumba cha mtihani mtapata adhabu kali ikiwemo kufutiwa mtihani!

Katika maisha ya kawaida hasa ya kusaka fedha, unahitajika ushirikiano mkubwa sana, baina yako na wadau, wateja, wafanyakazi wenzio, marafiki n.k. Kwa kifupi unatakiwa kuwa na Networking ya kutosha.

 Huwezi kufika mbali kiuchumi kama utakuwa na "mentality" ya ubinafsi unaosisitizwa madarasani!

Simaanishi kusoma hakuna maana, isipokuwa ninakwambia: Kama ukipata nafasi ya kusoma, soma kwa bidii; lakini usibebe kila wanachokulisha madarasani; ukakileta huku mtaani.

Mtaani panahitaji akili ambayo ni tofauti na hiyo iliyopimwa kupitia kukariri ya vitabuni, mwishoni wanakuzawadia makaratasi yaitwayo vyeti.

Ukitaka kufanikiwa ungana na waliofanikiwa wakuelekeze.

😡 UKWELI MCHUNGU!!

Jumanne, 19 Julai 2016

ILI UFANIKIWE FUATA NJIA HIZI



Maisha uliyonayo sasa ni matokeo ya maamuzi unayoyafanya kila siku kwenye maisha yako. Maamuzi yoyote unayoyafanya kila siku, yana uwezo wa kufanya maisha yako ya kesho kuwa mazuri au mabaya.

Kwa mfano, upo hapo na maisha yako hivyo kwa sababu ya maamuzi kadhaa ambayo ulishawahi kuyafanya kipindi cha nyuma. Maamuzi yako uliyokuwa ukiyafanya iwe kwa kujua au kutokujua ndiyo yaliyokufikisha hapo.

Kwa hiyo unaona ili kufanikiwa, maaumuzi mazuri ni kitu cha msingi sana. bila kuwa na maamuzi ya msingi itakuwa ni ndoto kubwa kufikia mafanikio. Ndio maana kila wakati unatakiwa ujiulize maamuzi ninayo yafanya sasa yanajenga maisha yangu au yanabomoa.

Ukishajua aina ya maamuzi sahihi unayotakiwa kuyafanya itakusaidia sana kubadilisha maisha yako. kwa kawaida wengi huwa ni watu wa kuharibu maisha yao kwa kufanya maamuzi yasiyo na miguu wala kichwa. Kwa kifupi wanafanya maamuzi yanayo wagharimu sana.

Ili kufanikiwa tunaona, ni lazima kujijengea maamuzi sahihi yanayokuongoza kwenye mafanikio. Kupitia makala hii leo, tutajifunza aina ya maamuzii ambayo ukiyafuata kila wakati yatabadilisha misha yako kabisa. Je, ni maamuzi yapi sahihi unayotakiwa kuyafata ili yakupe mabadiliko ya kweli?

1. Uamuzi wa kuchagua kufikiri.
Tatizo walilonalo watu wengi ni watu wa kuwaza tu na sio kufikiri. Naona unashangaa unawaza naongea kitu gani? Sikiliza, ipo tofauti kubwa kati  ya kufikiri na kuwaza.

Kufikiri ni mchakato unakufanya ukupe majibu juu ya suluhisho la matatizo yako. Unapokuwa unafikiri unakuwa unaweza ni nini ufanye ili uwaze kufanikiwa au kutoka kwenye hali ngumu uliyonayo.

Lakini unapowaza, unakuwa hutafuti sana suluhisho la mambo yako, zaidi unakuwa unaongozwa na matukio ya kawaida. Sasa ili uweze kufanikiwa ni lazima sana kwako wewe kufikiri na kupata majibu ya kie unachokitaka.

Ni muhimu kuchagua kufikiri kwa sababu hiyo itakupa mafanikio makubwa. Jiulize binafsi unafikiri au unawaza tu. Kama unawaza tu, elewa kufikia mafanikio yako itakuwa ni ngumu sana.

2. Uamuzi wa kuchagua kile tunachokizingatia.
Kile unachokizingatia sana kwenye akili yako ndicho unachokipata. Hauwezi kupata kitu ambacho hujakiweka kwenye akili yako. Kila wakati angalia ni kipi unachokizingatia sana na kukiwaza kila wakati kwenye akili yako? Kwani hicho bila shaka ndicho utakachokipata bila wasiwasi.

Unaweza ukawa shahidi katika hilo, hebu angalia yale mambo yote uliyoyatimiza kwenye maisha yako. Ukifatilia utagundua kwamba mambo hayo uliyazingatia sana kwenye akili yako kwa namna moja au nyingine ndiyo uliyoyapata. Hivyo, ni muhimu kuwa na uamuzi wa kuzingatia kile unachokitaka, utakipata hicho.

3. Uamuzi wa kuchagua kupanga mipango bora.
Kuchagua kufikiri vizuri na kuchagua kile tunachikizingatia hiyo peke yake haitoshi. Ili kuweza kubadilisha maisha yako kabisa pia unatakiwa pia kujiwekea mipango bora. Ni lazima kuweza kukaa chini na kupanga  kitu gani ni unachokitaka katika maisha yako.

Ukiishi tu kiholela bila kujiwekea mipango mizuri hiyo itakusumbua sana hata kufikia mafanikio yako makubwa. Watu wenye mafanikio makubwa ni watu wa kuishi kwa mipango mizuri ambayo badaae huamua kuisimamia mpaka itimie.

4. Uamuzi wa kuchukua hatua.
Kupanga mipango mizuri pekee hakutasaidia kama hatua sahihi hazitachukuliwa. Hivyo, hatua ni kitu cha muhimu sana ambacho kila wakati unatakiwa kukizingatia ii kuweza kufanikiwa. Bila kuzingatia kuchukua hatua kwa hakika hiyo inakuwa ni sawa na kazi bure.

Kumbuka kwa kuzingatia kila wakati uamuzi wa kuchagua kufikiri, uamuzi wa kuchagua kile tunachokizingatia, uamuzi wa kuchagua mipango bora na uamuzi wa kuchukua hatua dhidi ya maisha yako, hiyo itakusaidia sana kwako wewe kuweza kufanikiwa na kubadilisha maisha yako

HII NDIO SABABU YA DAGAA WA KIGOMA KUUZWA BEI GHARI



KAMA ukibahatika kutembelea katika masoko mbalimbali nchini bei ya Dagaa Ndagala maarufu kama Dagaa wa Kigoma mara nyingi imekuwa juu ikilinganishwa na dagaa wengine.

Dagaa hao ambao wanapatikana katika Ziwa Tanganyika wanapendwa na watu wengi na sifa kubwa ya kitoweo hicho ni kutokuwa na mchanga.

Kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma, wengi wanaendesha maisha yao kutokana na kuuza kitoweo hicho ambacho kimekuwa kikisafirishwa na kuuzwa katika maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani kama za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Vijiji vya Ibirizi, Mwamgongo, Nkonkwa, Lagosa na Katumbi ambavyo viko katika mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma ni maarufu kwa kufanya biashara hiyo ya dagaa.

Katika vijiji hicho makundi ya wanawake na vijana wamejiajiri katika biashara hiyo na wengi wanakiri kwamba imewasaidia kuendesha maisha yao na familia zao.

Gazeti hili lilizungumza na wafanyabiashara na wavuvi ili kujua siri ya mafanikio hayo.

Mmoja wa wafanyabiashara hao kutoka Kijiji cha Katumbi, Salama Athumani, anasema dagaa hao huandaliwa katika mazingira masafi na kuwafanya kuwa bora zaidi.

“Ni nadra mtu kula dagaa wa Kigoma halafu wawe na mchanga na kama ikitokea ni mara chache labda mtu aliokota waliodondoka chini na kuchanganya na wengine,” anasema Salama.

UKAUSHAJI

Kwa kiasi kikubwa samaki wadogo (dagaa) huuzwa wakiwa tayari wamekaushwa lakini jamii nyingi za wavuvi awali zilikuwa zikitumia mbinu ambazo hazikuwa salama kiafya ambazo zilichangia kupunguza ubora wa kitoweo hicho kutokana na kuharibika pamoja na upotevu wa samaki.

Katika maeneo ya Afrika inakadiriwa kuwa samaki wanaoharibika kabla ya kumfikia mlaji ni kati ya asilimia 20 hadi 25 na wakati mwingine hufikia asilimia 50.

Ofisa Uvuvi Mwandamizi kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, John Mapunda, anasema kutokana na ongezeko la watu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, mahitaji ya samaki yameendelea kuongezeka siku hadi siku, hivyo kusababisha uzalishaji samaki kutoka kwenye vyanzo vya asili kupungua kwa kasi.

TEKNOLOJIA YA KICHANJA

Shirika la Chakula Duniani (FAO), lilitoa Waraka wa Kuzingatiwa wa Uvuvi Endelevu (Code of Conduct for Responsible Fisheries) unaosisitiza umuhimu wa kupunguza upotevu wa samaki.

Pamoja na waraka huo Shirika hilo lilikuwa linatekeleza mradi katika jamii za wavuvi wa samaki ndogondogo zilizoko katika Ziwa Tanganyika, nchini Burundi.

Mradi huo ulijikita katika kuleta mbinu za gharama nafuu za ukaushaji dagaa kwa kuanika kwenye kichanja ili kuhakikisha kitoweo hicho kinakuwa salama na kuwa na soko zuri.

Mbinu ambayo imeonekana kuwa na manufaa makubwa hivi sasa imesambaa hadi katika vijiji vilivyoko mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.

Patiasi Deo ambaye ni mfanyabiashara katika Kijiji cha Lagosa, anasema ubora wa kitoweo hicho unatokana na uandaaji wake aliodai kuwa ni wa kimataifa.

“Walikuja watu wakatufundisha kukausha dagaa kwa kuwaweka katika vichanja badala ya kuanika chini. Zamani tulikuwa tunaanika chini halafu wakikauka tunawachekecha lakini mchanga ulikuwa hautoki wote.

“Yaani ukianika chini mchanga, mvua na matope huharibu matokeo yake unaweza kujiharibia soko kwa sababu mtu akinunua akakuta wana mchanga anaweza asirudi tena kwako,” anasema Joseph.

Mfanyabiashara mwingine kutoka katika Kijiji cha Mwamgongo, Ismail Juma, anasema ukaushaji dagaa kwa kutumia vichanja umeimarisha usafi na usalama wa dagaa hao.

“Tangu tuanze kukausha dagaa kwenye vichanja bei imepanda na imekuwa ni faraja kwetu wafanyabiashara na wavuvi,” anasema Juma.

Juma anasema huwa wananunua dagaa wabichi kwa Sh 12,000 kwa karai moja ambapo baada ya kukaushwa hupatikana kilo tano. Katika eneo hilo kilo moja huuzwa kati ya Sh 8,000 hadi 10,000 kutegemeana na msimu.

Kwasasa bei ya Dagaa Kigoma katika masoko ya jijini Dar es Salaam ni kati ya Sh 23,000 hadi 25,000.

“Kwasasa dagaa wanapatikana kwa wingi kwa sababu huu ni msimu wake, lakini kuna wakati wanakuwa wachache kwahiyo lazima bei itakuwa juu tu,” anasema.

Ripoti ya FAO iliyotolewa mwaka juzi inayoonyesha kuridhishwa na mradi huo kwani pia umesaidia kutunza rasilimali za ziwa Tanganyika.

Ofisa wa FAO Yvette Diei Ouadi, anasema waliwasaidia wavuvi kutengeneza chanja za kukausha zilizo juu kidogo na zenye kifuniko ili kuzuia mvua na kwamba baada ya muda mfupi vijiji vingine vilianza kuiga mbinu hiyo.

Kabla ya kuja mbinu hiyo asilimia 15 ya samaki waliokamatwa walikuwa wanapotea au wanaharibika wakati wa kukaushwa.

COSTECH, TAFIRI

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi nchini (TAFIRI), hivi sasa wanatekeleza mradi unaolenga kutumia teknolojia nafuu na rafiki wa mazingira katika ukaushaji wa samaki katika vijiji vilivyoko mwambao wa Ziwa Nyasa.

Wastani wa tani 30,000 huvuliwa kwa mwaka kutoka Ziwa Nyasa huku upotevu wa samaki hasa wakati wa mvua hukifikia hadi asilimia 50 ya samaki waliovuliwa na hasa kwa samaki wadogo. Upotevu hutokana na desturi za ukaushaji samaki kwa kutumia moshi au kwa kuanika mchangani.

TAFIRI kwa msaada wa fedha kutoka COSTECH imeboresha makaushio ya gharama nafuu yanayotumia nishati ya jua kwa ajili ya ukaushaji wa samaki wadogo wadogo.

Mradi huo ulianza mwaka 2013 ukiwa na lengo la kuboresha mbinu za matumizi ya nishati ya jua katika kukausha samaki kwa kutumia makaushio au majiko yanayotumia nishati ya jua.

Majiko hayo yanatumia vifaa vinavyopatikana kirahisi katika mazingira husika. Yapo makaushio ya hema, boksi, shimo na meza ya wazi ambayo hufanya kazi kwa kuzingatia uwezo wa kuhifadhi joto na unyevu nje na ndani, mwendo kasi wa upepo wa nje, kasi ya ukaushaji na muda wa bidhaa kudumu bila kuharibika baada ya kukaushwa.

Sampuli za samaki wakavu waliochakatwa zilipelekwa kwenye maabara za Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) ili kuchunguza viinilishe na madini na aina ya kaushio la hema limeonyesha kufanya vizuri zaidi ikilinganishwa na makaushio mengine.

FAIDA ZA DAGAA

Dk. Willy Sangu kutoka Manispaa ya Ilala, anasema dagaa ni chanzo cha madini ya chuma mwilini. “Ni chakula bora kwetu sote ambacho kinaweza kuliwa na wali, ugali, ndizi za kuchemsha, mihogo, viazi na vyakula vingine.”

Kwa ujumla teknolojia hiyo ya ukaushaji dagaa ni nafuu na imechangia ubora wa kitoweo hicho kuongezeka siku hadi siku na kuboresha kipato cha wavuvi, wachakataji na wafanyabiashara ya samaki katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, hivyo ni muhimu ikaendelezwa katika maeneo mengine.

Jumatatu, 18 Julai 2016

MANGU:TUTAMSHTAKI MAALIM SEIF



MKUU wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu amefunguka kuhusu mambo juu ya utendaji wa jeshi hilo na kueleza kuwa wakati wowote litamburuza mahakamani Katibu Mkuu wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuhamasisha uchochezi visiwani Zanzibar.

Amebainisha kuwa jeshi hilo, kamwe halikandamizi wala kuonea chama chochote cha siasa, kwani limekuwa likitekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.

Akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika kwenye kipindi cha Funguka, kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Azam jana, IGP Mangu alisema hali ya siasa Zanzibar ilikuwa shwari katika chaguzi zote mbili na kwamba machafuko na vurugu vilianza kutokea baada ya uchaguzi wa pili.

Alisema vurugu hizo zilianza baada ya kubainika kuwa Maalim Seif, alikuwa akifanya mikutano ya ndani na mingine ya chini kwa chini na wafuasi wake katika maeneo ya Kaskazini na Kusini.

“Kwa sababu ilikuwa ni mikutano ya ndani, Polisi hatukuona tatizo na wala hatukumzuia, tuliona ni mwananchi anataka kuzungumza na wafuasi wake, tukasema mwache aongee nao tu,” alisema IGP Mangu.

Alisema baadaye jeshi hilo liligundua kuwa kiongozi huyo wa CUF, alikuwa anawachochea wananchi waichukie serikali iliyopo madarakani na wapinzani wao ambao ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwafanyia uhalifu.

Alisema baada ya vikao hivyo vya Maalim Seif, visiwani humo kukaanza kuibuka matukio ya vurugu kama vile mashamba kuchomwa moto na mazao kung’olewa.

“Haya mambo hayakutokea kabla ya vikao vya Seif, yalitokea baada ya vikao vyake,” alifafanua mkuu wa polisi.

Alisema wafuasi hao walichochewa, kiasi cha kususa hadi shughuli za kijamii, kama vile misiba na wakati mwingine ilifikia hatua ya kususa kuwauzia bidhaa wafuasi wa CCM.

“Tukasema kama wameona kugeuza biashara zao siasa, basi waendelee tu. Biashara inadumu kwa sababu unatengeneza faida, sasa kama umeamua kuchagua wa kumuuzia ni shauri yako. Hawa tuliwaacha kwa sababu tuliona hawana makosa,” alisema.

Hata hivyo, alisema jeshi hilo kamwe halikuwanyamazia wahalifu waliochoma na kung’oa mazao kwenye mashamba ya wenzao, eti tu kwa kigezo cha ufuasi wa chama au siasa.

“Hawa tuliwakamata na wapo wengine tunaendelea kuwatafuta, watakapoacha ndio hatutawatafuta. Wale wahalifu ndio tunaowatafuta. Pengine kwa sababu ya siasa wanadhani Polisi tunawaonea wananchi tunawakamata bila sababu. Sasa hawa watu tunawaoneaje wakati tunawapeleka mahakamani?” Alihoji.

Maalim Seif kuhojiwa Alisema kutokana na matukio hayo, tayari Maalim Seif amehojiwa na jalada lake halijaamuliwa, lipo kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) Zanzibar. “Lakini pia tunataka tumpeleke mahakamani kumshitaki kwa makosa aliyofanya ya kuchochea fujo,” alieleza.

Alisema kazi kubwa ya Polisi kwa sasa si kujiingiza kwenye siasa au kupatanisha pande mbili zinapokwaruzana, bali kazi yake ni kuhakikisha inadhibiti na kuwakamata wahalifu.

Alisema endapo vyama viwili vinavyolumbana visiwani Zanzibar, vitaamua kuchukua hatua za kisheria kumaliza tofauti zao, polisi haina tatizo, lakini endapo vyama hivyo vitachukua hatua za kijinai au kukomoana, jeshi hilo halitokaa kimya.

“Kazi ya polisi iko wazi, tunakamata tunapeleleza na kupeleka mahakamani umma unatuona tunachofanya hatuna cha kuficha,” alisisitiza.

UVCCM YAWASAKA VIJANA WA CHADEMA (BAVICHA),DODOMA



KAIMU Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka amewasili mkoani Dodoma na kuhoji waliko vijana wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) waliotangaza kutaka kuuvuruga Mkutano Mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii.

Shaka alisema yuko mkoani hapa kwa ajili ya kuongoza harakati za kukilinda chama hicho kwa kushirikiana na vijana wa CCM.

Alisema UVCCM imeandaa vijana 30,000 maalumu kwa ajili ya kulinda mkutano huo utakaohudhuriwa na viongozi wote wa juu wa serikali na CCM.

Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema aliwasili mapema mkoani Dodoma ili pamoja na mambo mengine ashuhudie vurugu zilizoahidiwa na Bavicha lakini, hadi sasa hakuna chochote.

“Nipo hapa kwa muda mrefu kwa ajili ya kuongoza shughuli za ulinzi wa chama na viongozi wetu nikiwa mtendaji mkuu na mtoa maelelezo ya kiitifaki.

“Kwa bahati mbaya kwa muda wote huo sijaona dalili wala hata harufu ya Bavicha. Hii inadhihirisha kwamba kusema na kutenda ni vitu tofauti,”alisema Shaka.

Alisema azma ya UVCCM ilikuwa ni kuithibitishia dunia kwamba Watanznia hawako tayari kuona kundi lolote la wahuni likichafua amani, utulivu na usalama wa watu na likaachwa litambe  bila kufundishwa.

Shaka alisema, wajumbe wa mkutano huo hawapaswi kuwa na hofu juu ya usalama wao na mali zao na kuwaomba waingie Dodoma wakiwa na  imani na watatoka salama kwa kuwa vijana wa kuwalinda wapo wa kutosha.