Jumatano, 23 Mei 2018

HATUA KUU TATU ZA KUFIKIA NDOTO YAKO


Unaweza kushangaa kwa nini hupati kile unachokitafuta!Je unajua sababu ya kushindwa kutimiza ndoto zako ni wewe mwenyewe?
Utakubaliana na mimi kuwa sababu ya kushindwa kutimiza ndoto zako ni kwa sababu haujui nini unakitafuta na unakihitaji.

Watu wengi wamekuwa na hamu ya kupata mafanikio makubwa lakini wameshindwa kutofautisha hamu/shauku zao ambazo zimegawanyika katika viwango vitatu vya uhitaji.

Viwango hivi vitatu ambavyo vitakusaidia wewe kujua upo katika kiwango gani,pengine kupiga hatua kutoka katika kiwango ulichonacho kwenda kwenye kiwango kinachofuata

1. KIWANGO CHA "NINGEPENDA"
"Ningependa" neno hili huonyesha upenzi wa kitu fulani ambacho mtu anapenda kukipata au kuwa.Mfano Ningependa kuwa raisi,Ningependa kuwa tajiri.,,

Ningependa kuwa mfanya biashara mkubwa.Watu wengi wako katika kundi hili la kutaka kuwa mtu fulani lakini katika kundi hili hutumika nadharia tu, hakuna kitendo chochote kitakachotokea katika kiwango hiki cha kupenda.


2. KIWANGO CHA "KUTAKA"
Katika hatua hii watu husema nataka kuwa mtu fulanii ninataka kuwa mwandish mzuri,ninataka kuwa mwalimu mzuri.

Hatua hii inakusanya maandalizi madogomadogo pia ni hatua muhimu ya mwanzo inayokusanya vitendea kazi kwa ajili ya kuvitumia katika kusudio lako.

Kiwango hiki sio kiwango ambacho kinakuweka katika kilele cha mafanikio lakini ni kiwango cha pili cha muhimu cha maandalizi ya kukuweka kwenye kilele.

3. HATUA YA KUJITOA (KUFANYA KAZI)
Katika hatua hii ndipo watu huanza kufanya kile ambacho ndoto yao inataka iwe,bidii ndio funguo muhimu ambayo mtu anapaswa awe nayo katika kufanikisha jambo lake na kupiga hatua zaidi.Dhamira ndio kiini cha mambo yote kwa kunafanya kile ambacho umekidhamiria,kile ambacho kimekuwa ni ndoto yako ya kila siku.

Dhamiria kikamilifu katika ndoto zako,fanya kazi kwa bidii bila kuchoka,weka mipango na mikakati ya kuendeleza na kupanga ndoto zako hakika utakuwa umepiga hatua kubwa kimaendeleo na utaweza kufikia malengo yako na kupata kile unachkitafuta.

Ukawe na siku njema msomaji wangu wa mtandao wa www.patamamboadress.com
Ni mimi Mwandishi wa makala hii Bundala Izengo.a

Jumapili, 21 Januari 2018

HIVYO ULIVYO NI ZAO LA MAWAZO NA TABIA YAKO



Ni tumaini langu kuwa haujambo rafiki yangu mpendwa na msomaji wa blog hii ya patamambo,leo katika makala haya ninakwenda kuangazia nguvu ya MAWAZO inavyoweza kubadilisha maisha yako hata ulimwengu.

Wazo ni nguvu ambayo imeleta mabadiliko makubwa katika dunia hii,uumbaji wa dunia na mali zote zilizopo ulianza na wazo.Mungu alimuumba Adamu baada ya kumuumba Adamu Mungu ALIWAZA Haipendezi mtu huyu kuishi peke yake ndipo alipompatia msaidizi wake ambaye kwa jina aliitwa Hawa.

Huu ni moja wa mfano ambao nimekupatia ndugu ili uelewe juu ya Nguvu ya Wazo ambavyo imekuwa tangu dunia kuumbwa.Wagunduzi wa sayansi na tekinolojia wote walianza na wazo kisha wazo hilo wakaliweka katika vitendo ndio maana leo tuna simu za mkononi,ndege,mitandao ya kijamii nk.

Je una wazo gani hapo ulipo,wazo lako lina nguvu,Wazo lako lina uwezo wa kukufikisha katika uhuru kifedha,Je wazo lako unaweza kuliweka katika uhalisia na kulifanyia kazi ili likuletee faida na kukupatia kipato?Haya ni maswali unayopaswa kujiuliza kabla ya kuliweka wazo lako katika vitendo.

Maisha yako yanaaksi mawazo yako uliyowaza mwaka uliopita,miezi iliyopita,juzi,jana na leo,maisha uliyonaho sasa umeyatengeneza kwa mawazo yako ya siku za nyuma kwa kujua au kutokujua,nguvu ya wazo lako ndio maisha ambayo unayoyaishi sasa na utaendelea kuyaishi kesho na kesho kutwa.

Sikiliza Rafiki nikuambie Kushindwa sio kitendo cha siku moja,huwezi kushindwa kwa usiku mmoja, kushindwa ni kosa ambalo unalifanya katika mawazo yako ni tabia ya kurudia rudia kosa kila siku hivyo matokeo yake sasa kosa hilo linakuletea matokeo hasi juu ya wazo lako.

Hivyo ulivyo ni zao la mawazo na tabia au matendo yako ambayo unayarudia rudia kuyafanya kila siku.Wewe ni maskini kwa sababu hauna tabia ya kuweka akiba kila mara,ni maskini kwa sababu mawazo yako hayaendani na vitendo vyako vya kila siku.

Asante sana kwa kusoma makala haya ni mimi Bundala A. Izengo 0656669989

Jumamosi, 20 Januari 2018

FANYA HAYA ILI UWEZE KUFIKIA MALENGO YAKO MWAKA 2018



Kwaheri mwaka 2017 karibumwaka mpya wa 2018 hizi ni baadhi ya sauti za watu wengi ambao Mungu amewajaalia kuona mwaka Mpya.
Nianze kwa kukuambia kuwa Hongera sana rafiki kwa kuona mwaka 2018.

Kila mwanzo wa mwaka watu hupanga mipango mingi ili kuweza kusukuma maisha ya kila siku na kutimiza ndoto mbalimbalimbali.Ni vyema ndugu ukawa na mipango ambayo utaenda kuifanyia kazi mwaka huu 2018 na hakikisha kuwa mipango hiyo inafanikiwa kabla ya kumaliza mwaka 2018.

Rafiki unapoanza mwaka mpya kitu pekee kinachobadilika ni namba yaani 2017 - 2018 mambo mengine yote hubaki kama yalivyo,thamani ya pesa hubaki vilevile,masaa huhesabika vilevile,Dunia hulizunguka jua katika staili ileile,pumzi na hewa tunayovuta huwa ni ileile n.k.

Katika mwaka huu 2018 kitu pekee unachopaswa kubadili ni staili ya maisha uliyonayo unahitaji mabadiliko ya kifikra katika kufikia mafanikio yako, unahitaji mabadiliko ya kiroho ili kufikia malengo yako, unahitaji mabadiliko ya kimwili ili kuweza kufikia malengo yako,pia unahitaji kubadili mbinu za kuongeza thamani na faida katika biashara yako au kazi yako ili kweza kufikia malengo yako.

Unapoanza mwaka 2018 unakuwa na uhakika wa asilimia mia (100%) wa kufikia malengo yako,kadri siku zinavyokwenda ndivyo asilimia inavyozidi kupungua.

Mpaka kufikia tarehe 30/12/2018 wapo watakao kuwa wamepunguza asilimia zao za kufikia malengo na kufikia 80,70,10,20,95 hata wengine 98%.

Ningependa kila rafiki yangu katika mtandao huu anafikia malengo yake mwaka huu 2018 bila kujali ukubwa wa malengo hayo.

Fanya haya
1.Chukua Daftari andika malengo yako kumi unayofikiria kuyatimiza mwaka huu.
2. Chambua malengo yako Matano
3.Chambua tena malengo mengine matatu muhimu.
4. Andika lengo lako muhimu moja ambalo utaenda kulifanyia kazi kila kukicha.

Jikumbushe malengo yako muhimu matatu kila siku na ufanyie kazi lengo lako moja kila siku bila kusahau malengo yako mawili muhimu ambayo nayo utayafanyia kazimwaka huu 2018.

Fuatilia blog hii Patamambo ili tuweze kuhamasishana kila siku.

"USIKU HUU WANAITAKA ROHO YANGU"



Aliingia mkuu wa wachawi ambaye alikuwa akitokea Gamboshi iliyoko mkoani shinyanga wilayani Bariadi, kila mchawi alisimama na kuanza kupiga makofi kwa staili ya aina yake,walikunja mikono yao na kufanya kama kuku anayegonga mabawa akitaka kuwika.
Mkuu wa wachawi aliingia akiwa na ungo alitembea kwa kila aina ya madaha huku akifuatiwa na walinzi wake, alitokea mchawi mmoja ambaye alikuwa amebeba mtu ambaye Nipe alimfahamu.Alikuwa ni jirani yake ambaye ni mwenyekiti wa kijiji hicho,mama huyo alikuwa ni mnene na alikuwa na makalio makubwa.

Mkuu wa wachawi alikaa katika makalio ya mama yule ambaye aliwekwa chini na kuanza kikao.
“kwanza kabisa poleni kwa kazi pevu ya kulijenga taifa hili la kichawi ambalo linaongeza mamilioni ya wajumbe, si viongozi wa kisiasa ,watoto ,wakubwa hata maadui zetu wachungaji wametupa biblia na kujiunga na taifa hili.” Alizungumza kwa kujiamini.

Jicho la nipe lilikuwa likimtizama mama yake ambaye alikuwa akiitikia kwa shangwe na kila aina ya furaha .
Sina alikuwa akipika na mabinti wenzake wawili ambao walikuwa wamehudhulia kikao hicho.

Siku hiyo ilikuwa siku ya kufunuliwa kwa Nipe kwani dada zake wote walifariki katika mazingira ya kutatanisha .Baada kuzungumza kwa muda mrefu mkuu wa wachawi alisimama na kuzungumza kwa sauti ya hamaki.

“Nimepata taarifa kuwa kuna mshiriki mwenzetu ambaye alikuwa akipiga chenga ya kutoa kafara yetu ambayo tumejiwekea tangu enzi za mababu zetu, nimekuja kusikiliza malalamiko hayo ambayo leo tutayapatia ufumbuzi.” Mama yake Nipe alivuta pumzi kwa uoga.

“Mkuu hilo lilikuwa likitusumbua katika kambi yetu hii takatifu,mama Nipe amekataa kutoa kafara amekuwa akikataa kwa sababu amebakiwa na mtoto mmoja tu.”alizungumza mmoja wa wachawi aliyekuwa karibu na mama Nipe.

“Naomba tumpatie nafasi ya mwisho siku ya leo atupatie nyama au damu ya mtu ya kutupatia nguvu na kuimarisha uchawi wetu.unayo nafasi mama Nipe tupe mtu ili leo tupate chakula chetu.” Alizungumza mkuu wa wachawi ambaye alikuwa msuluhishi wa migogoro katika matawi ya serikali ya wachawi hapa nchini.

“Mkuu leo sina la kuzungumza zaidi ya kutoa karafa hiyo,kwa heshima na taadhima naomba vijana wako waelekee kwangu katika chumba cha Nipe wakamchukue kwa ajili ya kitoweo katika kikao hiki kitakatifu.”
Wote walishangilia,vijana watatu wenye miraba minne walitumwa kumchukuwa nipe nyumbani kwao kwani mama yake aliamini kuwa atakuwa karudi kutoka kwenye ngoma ya chagulaga.

Vijana hao walisimama na kuchukua usafiri wa ungo,alikimbia kwa spidi kuliko umeme, Nipe alikuwa juu ya mti wa mkwaju akisikiliza kila kilichoendelea,alishtushwa aliposikia mama yake kimtaja kuwa afuatwe ili auwawe.

“kweli mama anazungumza ili mimi niuwawe!”alizungumza kwa mshangao mkubwa huku akitetemeka miguu na mikono hali ambayo matawi ya mkwaju yalianza kutikisika ,Sina aliona hali hiyo na kujisemea kwa sauti kubwa

“Usiogope,kuwa na ujasiri”Mabinti wenzake waliokuwa wakisaidiana naye walimuuliza alikuwa ukizungumza na nani, lakini sina alisema alikuwa akikumbuka jinsi walivyokuwa wakiambiwa vijana wa kisukuma walivyokuwa wakicheza ngoma ya chagulaga.

Vijana waliotumwa walirudi mbio huku wakihema juu juu wakiwa mikono mitupu ,mama Nipe aliuliza kwa hamaki.

“ Yupo wapi mbona mnarudi mikono mitupu?”
“Hayupo tumemkosa kwani tumetazama kila kona ya nyumba tumemuona baba yake akiwa amelala lakini yeye hayupo” vijana walikuwa wametumwa kumfuata walijibu huku wakihema.

Mama nipe alichanganyikiwa alivuta pumzi kwa nguvu kabla hajaongea,mkuu wa wachawi aliuliza swali.

“Mama Nipe unataka kukichezea kikao tukufu cha wachawi ,umemficha mwanao eti” ilikuwa ni sauti ya kutisha ambayo ilionesha kuwa mkuu wa wachawi alikuwa kagadhabiika.Sauti hii iligonga katika ngoma za masikio ya mama Nipe na kumfanya apatwe na mshtuko.

“Nendeni mkamwangalie kwa rafiki yake Ngosha siku ingine huenda kulala huko .”Ilikuwa ni sauti ya mama Nipe ambaye aliamrisha vijana wake waende wakamwangalie Nipe kwa rafiki yake kipenzi ambaye hupenda kutembea naye mara kwa mara .

Vijana walichukua tena usafiri wao wa ungo na kupanda kila mmoja alihakikisha kuwa alikuwa yuko sawa sawia ndani ya ungo ule na kufyatuka.

Nipe alikuwa ndani ya mawazo mazito, mwili ulipigwa na ganzi alijikuta mkojo ukimtoka bila kujijua na kumdondokea bibi kizee aliyekuwa amekaa chini ya mti wa mkwaju.

“Haya maji yanatoka wapi”Aliuliza bibi aliyedondokewa na mkojo,sina hakuchewa kujibu.

“Bibi umekaa karibu na shina,wadudu na ndege hupenda kulala karibu ya shina atakuwa ni mdudu amekojoa .”Sina alizungumza na kumundolea kiti ambacho alikuwa amekalia na kukisogeza pembeni kidogo. Nini kitaendelea fuatilia blog hii

Jumatano, 25 Oktoba 2017

MTUHUMIWA NAMBA MOJA WA KIFO CHA UCHUMI WAKO NI WEWE



Nukuu "Maisha ni magumu na hayajawahi kuwa rahisi" Dr. Makrita

Nimeanza nakuandika nukuu ambayo itaniongoza katika makala haya ambayo nimekuletea siku ya leo.Nukuu hii ni ya Mwalimu wangu wa masuala ya ujasiliamali na uwekezaji Dr. Amani Makrita.

Mwanadamu ameumbwa na lugha ya lawama hasa kipindi anaposhindwa kutekeleza malengo yake,tumesahau ya kuwa matatizo ya kijamii na kiuchumi yapo kila siku, katika mazingira ya sasa utasikia neno hili

"Usawa huu wa Magufuli tutanyooka" Hizi ni sauti za watanzania wengi waliokosa tumaini la kesho na kujaribu kutoa lawama kwa Raisi aliye madarakani,ukitizama kwa mapana neno hilo linaashiria kuwa watu walitegemea kupewa pesa mikononi ama kupanga foleni kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa kwa ajili ya kupewa pesa,hata kama ingekuwa hivyo bado minong'ono juu ya hali ngumu ya maishi isingeisha.

Nadharia hii iko sahihi kwa asilimia 10 pia haiko sahihi kwa asilimia 90 ,serikali inatoa asilimia 10 tu kama mchango wake katika maendeleo ya kila mwananchi.Asilimia hizo kumi hutolewa kwa kupunguza bei za pembejeo na madawa,vitendea kazi,usalama wa raia na mali zake, kusimamia soko la ndani ili kusiwepo na mfumko wa bei n.k

Hizi asilimia 90 unapaswa kuzitafuta wewe,Mafanikio ya malengo yako, yapo mikononi mwako mwenyewe.Hebu fikiria Ndugu yangu, matajiri wa dunia wana mali kedekede lakini mpaka kesho wanaendelea kutafuta pesa bila kuchoka.

Yawezekana kabisa tukalalamika kuhusu ugumu wa maisha, lakini wimbo huu tusimhusihe kiongozi,taasisi wala kampuni fulani kuwa ndio sababu ya ugumu wa maisha huu ni wimbo ambao kila mwana mafanikio aukatae na kuukemea kwa nguvu zote, yawezekana sisi wenyewe tukawa sababu ya hali ngumu ya maisha kulingana na sababu ambazo nitaziorodhesha hapa.

UVIVU WA KUFIKIRI NA KUTENDA
Nikiwa natafakari jinsi ya kuianza siku ya siku ile, nilitizama pembezoni mwa ukuta wa nyumba na kuona majani ya tikiti yaliyotanda kuzunguka ua, lililokuwa karibu na chombo nachotumia kutupa taka kabla hazijaondolewa na Manispaa.

Nilitizama kwa makini Tikiti lile niligundua kuwa kwenye shina lake limebeba watoto watatu (matikiti) yenye ukubwa saizi ya ngumi.

Wazo jipya la biashara lilijengeka kichwani kwangu,nilikimbia mara moja mpaka katika duka la Pembejeo za Kilimo na kununua mbegu bora za matikiti.

Nilinunua jembe na viroba ambavyo vilitumika katika kuandaa shamba la nyumbani,nilipanda mbegu za tikiti katika viroba ambavyo nilivipanga pembezoni kuzunguka nyumba, nilifuata maelekezo yote ya mtaalamu wa kilimo kama alivyonielekeza niponunua mbegu hizo,baada ya miezi mitatu nilivuna jumla ya matikiti 200 ambayo niliyauza kwa shilingi 3,000 kila moja na kupata jumla ya shilingi 600,000/= .

Kama mimi niliweza unasubiri nini,anza leo usisubiri kesho.
Huu mchezo wa Taifa wa kulaumu mtu hatupaswi kuendekeza na kuuendeleza kamwe,tambua ya kuwa wewe ndio mtuhumiwa namba moja katika kosa la kudidimiza afya ya uchumi wako.

Nikiwa katikati ya mazungumzo na baadhi ya vijana wa mtaani kwangu,Nilishtushwa na sauti ileile ambayo vijana wa sasa wanapenda kuitumia.Ally Aliniambia neno hili

"Magufuli kabana kweli ndugu yangu nitoe hata buku kumi!"
Hii ni sauti ya kijana mwenye nguvu ambaye hata kabla ya utawala huu sikuwahi kumuona akifanya kazi yoyote isipokuwa kukaa vijiweni kupiga soga na marafiki zake,huku wakisubiria kengele ya chakula nyumbani kwao
Nilimuuliza swali hili Ally.

"Unasema hali ngumu wala viongozi hawana msaada kwenu mbona Kaka yako Jummanne Jana alifungua biashara mbili mpya,Vipi kuhusu duka jipya la mangi alilofungua hivi majuzi?"Hawa ni baadhi ya watu waliofungua miradi mipya hivi karibuni,Je hawa watu wametoa wapi mitaji ? wakati tunaishi nao Tanzania,Raisi wetu mmoja,Mbunge wetu mmoja, Diwani mmoja sera moja ya nchi,ardhi moja na thamani ya shilingi ni moja?" Jibu lilikuwa
"Kaka michongo imekaa vibaya"

Kila mmoja anaweza kutengeneza kiza nene juu ya Maisha yake,lakini kila mmoja anaweza akatengeneza nuru nzuri katika maisha yake kwa kufanya kazi kwa uadilifu,uaminifu na kujituma ili kufikia mafanikio makubwa.


Bundala anakuambia.
" Usisubiri mafanikio kutoka serikalini, kama unahitaji kufanikiwa anza kuyatafuta mwenyewe,Mafanikio yako, yapo mikononi mwako."



Alhamisi, 28 Septemba 2017

KABLA YA KUANZA BIASHARA/KAZI MPYA FANYA HAYA KWANZA


"Hodi Hodi.....!" Ilikuwa ni sauti ya kijana Mike ambaye sikumtia machoni miaka mitatu iliyopita.
"Karibu sana Kijana Habari za siku nyingi"Ilikua ni sauti ya Bundala Izengo Mwandishi wa Makala haya baada ya kutembelewa na kijana Mike ofsini kwake.

Sura ya Mike ilionekana yenye huzuni,aibu hata asili yake ya kujiamini ilipotea,mikunjo ya ngozi yake na mapere katika paji la uso(chunisi) na ngozi iliyofubaa na kupoteza rangi yake ya asili vilinisababisha kutoa chozi la huruma kwa kijana huyu ambaye alikuwa ni jirani yangu pia rafiki yangu kibiashara.

Si kwa sababu ya maradhi la hasha,hii ni kwa sababu ya maisha magumu aliyonayo baada ya kuacha biashara aliyokuwa anaifanya na iliyokuwa ikimuingizia faida nono baada ya kuambiwa na ndugu zake kuwa kuna biashara ambayo ingemwingizia kipato kedekede,Sio dhambi wala kosa kuacha biashara uliyonayo bali ni kosa kubwa kuacha biashara inayokuingizia kipato bila kufuata taratibu zifuatazo.

1.FANYA UTAFITI WA KUTOSHA
Ni dhahiri kuwa Mike hakuzingatia kipengele hiki muhimu cha uanzishaji wa biashara,hata kama alikifanya basi ni kwa kiwango cha chini kabisa,kipengele hiki kinakusanya mambo mengi ikiwemo kuandaa Mpango wa biashara, ni vyema zaidi ukawashirikisha wataalamu wa mahesabu ya biashara ambao watakusaidia mambo mengi ya kufanya kabla na baada ya kuanza biashara.

2. ZUNGUMZA NA WABOBEVU KATIKA BIASHARA HIYO
Hii ni hatua muhimu kabla ya kuanza kufanya biashara mpya waulize wenyeji wa biashara hiyo mambo mbalimbali yanayohusu biashara unayotaka kuifanya,ikiwezekana omba kazi mahali hapo hata kwa kujitolea ili uweze kujua changamoto za kazi hiyo japokuwa changamoto zingine hauwezi kuzijua mpaka utakapoingia rasmi kwenye biashara hiyo. Wakati hayo yote ukiyafanya usisahau kufanya hili lifuatalo ambalo Mike hakulifanya.

3. USIFUNGE BIASHARA YA MWANZO.
Ghafla Mike alipotea machoni pangu,duka lake akalifunga akawa anakuja kuchukua baadhi ya vitu na kuviuza kwa watu tena kwa bei ya hasara,nilijaribu kumuuliza ni kitu gani kimemkuta aliniambia maneno haya

"Huku mambo yametiki babu njoo tujichanganye kwenye biashara ya kuleta mazao ya viazi Mbatata jijini Dar es salaam" Sikukomea hapo nilijaribu kumshauri neno hili

"Mwachie mdogo wako au ajiri mtu aweze kukuendeshea biashara hii,huko uliko unawezakukwama ukarudi kwenye biashara yako ya awali."Mike alinitiazama kisha akacheka na kuniambia.

"Hapana Bundala,nafanya hivi ili kuongeza mtaji wangu kwani kiasi nilichonacho hakitoshi"Sikuchoka kumuuliza maswali ili niweze kujua faida inayopatikana katika biashara yake mpya,lakini nilipomujliza swali hili ndipo nikaumia zaidi
"Mtaji uliutoa wapi kijana mpaka ukaweza kufanya mambo makubwa kama haya?" Baada ya kunijibu swali langu hili,ndipo nilishangaa na kustaajabu ya Musa na baada ya miaka mitatu niliyaona ya Filauni, Majibu ya swali langu yalikuwa hivi.

4.USIKOPE ILI KUANZISHA BIASHARA MPYA
Watu wengi hufurahia kupata mkopo kwa sababu ni pesa ambayo unaipata bila ya wewe kuteseka wakati wa kuitafuta,sasa jua ya kuwa baada ya kukopa utateseka kuitafuta kwa ajili ya kurudisha mkopo.Kama tayari ulishaanza biashara yako na unataka kubadili biashara ni bora ukaweka akiba yako mpaka itakapojitosheleza.
Majibu ya swali langu yalikuwa ni hivi

"Nilikopa kwenye benki moja,kulingana na dhamana niliyonayo Walikubali kunipatia Milioni 10 hivyo ndio maana nimeanzisha niashara hivyo basi kutokana na ukubwa wa mtaji huo sioni sababua ya kuendelea kufanya biashara hii ya zamani"Alizungumza Mike na kuondoka.Niliwaza juu ya maisha aliyonayo wakati huo,niligundua ya kuwa, kwa mtaji huo Mike atakua ametusua (kufanikiwa).

5. HAKIKISHA UNA AKIBA YA KUTOSHA
Mwalimu wangu wa Ujasiliamali na Uwekezaji Dr. Amani Makrita,aliwahi kunifundisha somo hili ambalo ni muhimu sana endapo utadhamiria kuanza kufanya biashara mpya.Baada ya kupata mafunzo haya nilimkumbuka Kijana Mike Ambaye hakuweza kufuata kanuni hii pengine kwa kujua au kutokujua.Dr. Amani alisema hivi

Unapotaka kubadili biashara,hakikisha umeweka akiba ya kutosha katika akaunti yako,Hakikisha una pesa ya kuweza kuhudumia familia yako kuanzia chakula,malazi,mavazi na kulipia karo za shule kwa muda wa miezi sita ijayo,hakikisha una pesa ya kutosha ya kulipia madeni ya mikopo ya benki/binafsi kwa muda wa miezi sita bila kutegemea pato la biashara yako Mpya,uwe na akiba ya Nusu mtaji wako mpya kwa ajili ya kukabiliana na majanga au hasara.

Hili ndio lilikuwa kosa kubwa alilolifanya Mike ambaye aliingia katika biashara mpya akiwa na mkopo benki,bila ya kuweka akiba ya miezi sita ijayo.Baada ya kufanya biashara kwa muda wa miezi miwili Mike alipata ajari ya gari na kupoteza mali zake zote.
Maisha yaligeuka,alikimbilia kusikojulikana na kuacha mali zake Nyumba,kiwanja alizoweka dhamana zikachukuliwa na benki,Maisha yalikuwa magumu mpaka siku ha kwanza aliporudi mjini, nilijifunza mengi juu ya mkasa huu.
Nina imani unayesoma makala Haya hautaweza kufanya makosa kama ya Mike Jipange katika mambo hayo niliyokuorodheshea pindi unapotaka kufanya biashara Mpya au Kuacha kazi na kufanya kazi/biashara nyingine.

Hadithi hii ni ya kutunga haina ukweli wowote juu ya Maudhui na Majina. Mtindo uliotumika ni mtindo wa Darasa kwa njia ya hadithi.
Asanteni sana ni mimi BUNDALA ABELY IZENGO 0656669989

Jumatano, 6 Septemba 2017

MAMBO YANAYOSABABISHA MATUMIZI MABAYA YA PESA.


Kila kukicha matumizi ya pesa yanazidi kuongezeka hali ambayo inasababisha pesa iwe na majina mengi kama faranga,mshiko,mapene,ndarama,fulusi,senti,mbago,shekeli n.k.Kubadilika kwa majina haya si kwa bahati mbaya bali ni kwa sababu watu wanaipenda pesa na wanaitafuta pesa kila kukicha.

Unaweza kukubali kuwa kuitafuta pesa ni jambo moja na kuitumia pesa ni jambo jingine.Je ni wangapi wanaoitafuta pesa usiku na mchana wakiipata wanakwenda kuweka heshima baa?Je ni wangapi wanaotafuta pesa kwa jasho jekundu lakini matumizi yao yanaishia kwa madada poa?

Leo katika somo letu kwa njia ya hadidhi tutajifunza juu ya MAMBO AMBAYO YANASABABISHA MATUMIZI MABAYA YA PESA.
Katika familia tunazoishi matumizi mabaya ya pesa hurudisha nyuma maendeleo ya familia nilifanikiwa kusikiliza mzozo huu wa wanandoa hawa.

1. MATUMIZI YASIYO YA LAZIMA
"Hodi ndani" Ilikuwa sauti ya Bundala mwandishi wa makala haya alipomtembelea rafiki yake Shafii nyumbani kwake.
"Karibu baba mdogo"Sauti ya Jane (mtoto wa kwanza wa Shafii ilisikika ikinikaribisha) Niliingia ndani na kuketi juu ya kiti.
Ghafla nilisikia minong'ono iliyoashiria kuna shari chumbani kwa Shafii.

"Wewe unatumia vibaya pesa juzi umenunua Dela, Jana gauni leo unataka pesa kwa ajili ya kiatu wakati nguo na viatu unavyo tele!"Hii ilikuwa ni sauti ya rafiki yangu Shafii ambaye alikuwa akimgombeza mkewe kwa kumtuhumu kuwa anatumia vibaya pesa.

Uwepo wangu mahali pale nilihisi wa bahati mbaya,niliweweseka kimawazo na kushindwa kufanya uamuzi wa haraka,nilimtizama mtoto Jane alishindwa kuniangalia,mzozo uliendelea sasa haikuwa siri tena kwani sauti zilisikika kwa kila aliyekuwa karibu.

"Wewe kila siku unapanda boda boda ukitaka kwenda kazini na ukiwa unarudi mbona mimi sikuambii,unatumia shilingi elfu nne kila siku kwa ajili ya bodaboda ilhali ungeweza kutembea kwa miguu mpaka nyumbani si ungeweza kuokoa Laki moja na elfu ishirini (120,000/=) kwa mwezi?"Alihoji mkewe Shafii.

Umbali wa kutoka nyumbani mpaka barabarani ni mita mia mbili sawa na urefu wa viwanja viwili vya mpira.
Niliwaza juu ya hoja zao mbili ambazo zinaonekana dhahiri kuwa ni wivu wa matumizi mabaya ya pesa, nilipata jibu kuwa wote wana matumizi yasiyo ya lazima.

2: KUIGA TABIA ZISIZO NA MATOKEO MAZURI

Watu wengi hufanya kwa sababu wamemuona mtu flani anafanya,hivyo hupelekea kuishi maisha ya kuigiza kila siku,maisha haya hayana faida yeyote.Huwezi jua kwa nini yule anafanya hivyo yawezekana akawa na sababu ambazo wewe huzijui.

Mkasa wa Shafii na Mkewe uliendelea huku maskio yangu yakisikiliza kwa makini
"Nilishakuambia hao marafiki zako wanaokufundisha huu ujinga wa kuhudhuria kila harusi ya hapa mtaani sitaki kuwaona tena hapa nyumbani"Shafii alizungumza kwa hasira.

"Siwezi kuwaacha marafiki zangu nitaendelea kuwa nao na nitahudhuria sherehe kila napopata mwaliko,pesa ni ya kwangu,mshahara ni wangu halafu wewe unanipangia magumizi thubutuu"Ilikuwa ni sauti ya mke wa shafii ilisikika na kukatishwa ghafla.

"Hodi baba,baba mdogo amekuja" Jane alikuwa akimwita baba yake .

"Mkaribishe ndani"Baba yake alimjibu.

"Yupo amekaa kwenye kochi"Jane alimjibu baba yake huku akiusukuma mlango na kuingia chumbani kwa baba yake.

Shafii alitoka chumbani kwake na kuja sebureni,Sura yake ilijawa na aibu kiasi kwamba hata kunisalimu alipatwa na kigugumizi.

Nilimchangamkia ili niweze kundoa aibu aliyokuwanayo na niliyokuwanayo, Baada ya dakika tano kupita Shemeji(mkewe shafii) alikuja sebleni akiwa amefura na kifua kikiwa kimejaa hasira,hapo ndipo mambo yakawa hivi.(soma namba 4).

Ili uweze kufanikiwa ni lazima uachane na marafiki walio na fikra hasi juu ya maisha,wanaowaza kitchen party,vigodoro na mizimbao,walio na matumizi mabaya ya pesa,jiangalie wewe ulipo na unapokwenda kwani hakuna anayeweza kuubeba mzigo wako vijana wa siku hizi wanasema PAMBANA NA HALI YAKO.

4.KUTOKUWA NA BAJETI.

Bajeti ni muongozo wa matumizi ya pesa ambayo inakuwa imeandikwa katika karatasi,vifaa vya electronics n.k.Bila ya kuwa na bajeti kusingekuwa na mpangilio mzuri wa matumizi ya serikali,makampuni hata mtu binafsi.

Tunaendeshwa na bajeti ili kuweza kufikia malengo yetu tuliyojiwekea,kutokuwa na bajeti hatuwezi kufanya chochote wala malengo hatutayafikia.

Tukiwa tumekaa sebuleni walinieleza sababu ya ugomvi wao ambazo zililemea kwenye matumizi mabaya ya pesa katika mambo ambayo hayana umuhimu wala faida katika maisha yao.

Suala la bajeti ya pesa walizokuwa wanazikusanya lilikuwa ni shubiri kwao,kupelekea matumizi mabaya ya pesa na mara nyingine kukosa pesa ya chakula nyumbani na kusababisha madeni mengi na makubwa dukani kwa Mangi.

5. HISIA ZA KUPATA TENA KESHO

Hili ni suala ambalo watu wengi linawaathiri na athari zake zinakuja kuonekana hapo baadae,msemo wa tumia pesa ikuzoee umekuwa ni miongoni mwa misemo ambayo inaleta matokeo hasi katika maisha ya vijana wengi.

"Kwani shemeji nikipata mshahara wangu wa laki 5 kwa mwezi nikatumia laki 3 kwa ajili ya kununua nguo na mambo mengine,nikaweka laki 2 ya chakula nyumbani kuna ubaya gani?"Ilikuwa sauti ya Mke wa shafii ambaye alitaka ufafanuzi.
Swali hili limejengwa katika misingi ya "kesho nitapata hata kama nikitumia vibaya siku ya leo"Kitu ambacho ni sumu katika ustawi wa uchumi wa familia yako.

Pia maisha ya hawa wawili hayakuwa na mikakati kuhusu miaka 10 ijayo,bajeti zao zilikomea mwezi mmoja tena za kununua nguo za harusi.Maisha haya hautakiwi kuishi wewe unayesoma makala haya,Ishi maisha ya bajeti yenye matumizi mazuri ya pesa hapo ndipo utafikia uhuru kifedha.
Hadithi hii ni ya Kubuni haina ukweli wowote na majina yaliyotumika
Tembelea Blog Hii ya patamamboadress.blogspot.com

Mwandishi wa makala haya Bundala Izengo.0656669989