Jumatano, 10 Mei 2017

“USIKU HUU WANAITAKA ROHO YANGU”


Sina ni binti aliyekuwa akiishi na na baba,mama pia bibi katika Kijiji cha Sengerema mkoani Mwanza baada ya dada zake wawili kufariki dunia katika mazingira ya kutatanisa.
Sina alimpenda sana kijana aliyejulikana kwa jina la Nipe, Nipe ni kijana aliyekuwa na sifa zote za kumwita mtanashati kwani alipendeza kwa kila aliyemtizama.

Ilikuwa ni vigumu kwa Sina kugundua siri nzito aliyokuwa nayo mama yake,kila kulipokucha mama yake alikuwa akibeba jembe na kwenda shambani hata kama wakati wa kiangazi.

Siku moja kulitokea Ngoma inayojulikana kwa jina la Chagolaga maarufu sana usukumani.

Sina na Nipe walihudhuria katika ngoma hiyo ambayo ilipambwa na vijana wa kisukuma waliokuwa wamejifunga lubega kwa shuka la rangi nyeusi,huku vifua vyao vilikuwa wazi na waliokuwa wakicheza mchezo wa kuchapana fimbo, mabinti wa kisukuma walijifunga kipande cha nguo nyeupe kilichokuwa kimefunika matiti na kilichokuwa kimezunguka na kufungwa mgongoni.

Ulifika wakati wa kuchagua mchumba ambapo mvulana alikwenda kumchagua binti wa kike ambaye alikuwa karidhika naye. Mchezo huu hugeuka kuwa sumu na kusababisha kifo pale vijana wa kisukuma wanapogongana kwa binti mmoja hivyo hupigana mpaka kuonekana mshindi.

Siku hiyo ilikuwa ni burudani ya kutosha katika kijiji cha Sengerema,kila mahali kulikuwa na kundi la watu waliokuwa wakishuhudia tukio hilo ambalo huwa ni la kijadi,hufungisha ndoa vijana wa kisukuma pasipo na mkono wowote wa baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu wala wazazi.

Ngoja nikupe dondoo za Ngoma hii; Ngoma hii huchezwa na vijana wa kabila la kisukuma hasa wakati wa mavuno, vijana wa kiume huchagua binti ambaye atakuwa naye usiku ule,kama akimpendeza huchukua hatua za kuoa,naomba tukomee hapo manake naweza kuchukua siku nzima kuelezea mabaya na mazuri katika ngoma hii.

Ilikuwa ni usiku wa saa tatu,Sina na Nipe walianza safari ya kurudi nyumbani,  wakiwa njiani Sina alimwambia Nipe kuwa siku hiyo kuna kikao ambacho alihitajika kuhudhuria, aliendelea kumsihi kuwa asirudi nyumbani kwani kuna kitu kibaya kingemtokea hali ambayo angeweza kupoteza uhai.
Nipe alishangazwa sana na maneno, ambayo alishindwa kung'amua wala kutabiri killichotarajiwa kutokea usiku ule.

Alimwambia neno hilo kwa kumnong'oneza huku akimshika bega kwa msisitizo
"Usiku huu wanaitaka Roho yako".

“Unamaanisha nini mbona sikuelewi!”Nipe aliuliza kwa hamaki huku akiwa na shauku kubwa ya kujua ni kitu gani ambacho kingemtokea kama angelala nyumbani.
“Naomba unisikilize kwa makini mpenzi wangu Nipe. Mapenzi yangu kwako ni matamu kuliko hata sega la asali. Nakupenda sana ndiyo maana nakuomba usilale nyumbani."
"Kama utahitaji kuona basi twende katika mti ule wa ukwaju,ila ujue kuwa usiku huu wanaitaka roho yako.”

Ulikuwa ni usiku wa giza totoro,ulionakshiwa na manyunyu ya mvua na ngurumo za radi huku sauti za bundi zikisikika zikiashiria kuwa kulikuwa na kitu kibaya kilichokuwa kikiendelea.

Walisogea katika mti mkubwa wa ukwaju na kukaa chini Sina aliendelea kuzungumza.
“Nakupatia dawa hii jipake usoni”Sina alijipaka kama alivyoelekezwa
“Kisha panda juu ya mkwaju huu utakachokiona usishtuke kwani kutakuwa na kikao cha wachawi leo usiku nakuomba utulie kabisa kama unanyolewa”
Nipe alipanda juu ya mti wa mkwaju  na kutulia kimya ambapo alimwacha Sina chini akikusanya mawe ambayo yalitumika  kama mafiga ya kupikia.
Saa sita usiku iliwadia Nipe alikuwa juu ya mkwaju akipepesa macho kama kibaka aliyekuwa akimendea simu. Aliona fisi iliyokuwa akikimbia kwa kasi, mnyama huyo alifunga breki kali chini ya mti wa ukwaju, alipotizama kwa makini alimuona bibi kizee ambaye alikuwa ni jirani yake.

Bibi huyo alishuka kutoka juu ya Fisi huyo kwa staili ya aina yake, alitanguliza kichwa na kufuata kiwiliwili.
Haikupita hata sekunde kumi ziliingia Fisi mbili ambazo zilikuwa na mwendo mkali na kushusha wanaume wawili, haikuchelewa aliona fisi sita ambazo zilikuwa na ukubwa sawa na ndama nazo zilishusha akina mama na binti mdogo kabisa ambaye alimkadiria kuwa na miaka kumi na mitano.

Alipigwana butwaa alipomuona mama yake mzazi ambaye alikuja na usafiri huohuo na kushuka kwa staili hiyohiyo.

Nipe aliogopa sana moyo wake ulienda mbio hakuamini kabisa kama aliyemuona ni mama yake mzazi, alivuta picha ya nyumbani kwani kila siku mama yake hubeba jembe na kuelekea shambani kuchimba mizizi ya miti, alijikuta akiongea kwa sauti ya chini.
“Yawezekana mama akawa mchawi” Nipe aliendelea kutazama kilichokuwa kikiendelea chini ya Mkwaju huo.          

Aliingia mkuu wa wachawi ambaye alikuwa akitokea Gamboshi iliyoko mkoani shinyanga wilayani Bariadi, kila mchawi alisimama na kuanza kupiga makofi kwa staili ya aina yake,walikunja mikono yao na kufanya kama kuku anayegonga mabawa akitaka kuwika.
Mkuu wa wachawi aliingia akiwa na ungo alitembea kwa kila aina ya madaha huku akifuatiwa na walinzi wake, alitokea mchawi mmoja ambaye alikuwa amebeba mtu ambaye Nipe alimfahamu.Alikuwa ni jirani yake ambaye ni mwenyekiti wa kijiji hicho,mama huyo alikuwa ni mnene na alikuwa na makalio makubwa. NIni kitaendelea endelea kufuatilia kupitia blog hii.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni