Ijumaa, 22 Julai 2016

HALMASHAURI KUU CCM YAMPENDEKEZA DR.JOHN POMBE MAGUFULI KUWA MWENYEKITI WA CHAMA TAIFA



Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelipitisha kwa kauli moja jina Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, John Magufuli kuwa mgombea wa uenyekiti wa chama hicho

Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelipitisha kwa kauli moja jina Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, John Magufuli kuwa mgombea wa uenyekiti wa chama hicho akimrithi mtangulizi wake Jakaya Mrisho Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya CCM mjini Dodoma, Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi, Christopher Ole Sendeka amesema kuwa baada ya NEC kupitisha jina hilo ni wajibu wa Halmashauri kuu ya Taifa kuwasilisha jina hilo kwenye mkutano mkuu wa CCM utakaofanyika kesho kwenye ukumbi wa mpya wa CCM.

Ole Sendeka amesema kuwa ana imani na wajumbe wote wa mkutano Mkuu maalum wa CCM kuwa watampa kura za kutosha Dk, Magufuli kuwa mwenyekiti wa tano wa CCM tangu kuanzishwa kwake.

Awali akifungua kikao cha NEC Mwenyekiti wa CCM Dk, Jakaya Kikwete amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi kiko imara na kwamba kama hakikuvunjika mwaka 2015 hakitavunjika tena kutokana na mgawanyiko wa wanachama uliokuwepo katika kupata jina la mgombea urais kupitia chama hicho.

PANYA SASA KUTUMIA UZAZI WA MPANGO



CHUO Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kimepata suluhisho la kupunguza kuzaliana  panya nchini, kwa kuanzisha uzazi wa mpango kwa wanyama hao.

Akizungumza na waandishi Dar es Salaam jana, Mtaalamu wa Kilimo wa Chuo hicho, Thoneson Mhamphi alisema, utafiti huo ambao upo katika hatua za awali  haujaweza kusambazwa.

Mhamphi alisema dawa hizo za uzazi wa mpango zinazojulikana kama Quinestro na Levonorgester, zimekuwa zikichanganywa kwenye chakula na kuwapatia panya hao, hatua  inayowafanya washindwe kuzaliana.

“Huu utafiti ndiyo tumeanza kuufanyia kazi hivi sasa na   umeonyesha mafanikio kwa sababu  baada ya kuwapa chakula hicho panya hao wameacha kuzaana,” alisema.

Alisema dawa hiyo husababisha panya dume kuwa na nguvu ndogo ya kuzalisha kwa vile kizazi cha jike hujaa maji.

Mtaalamu huyo alisema panya wana  kasi ya kuzaliana ana anaweza kuzaa kila baada ya wiki tatu.

Vilevile, panya ana uwezo wa kupata mimba  tena  saa 24 baada ya kuzaa, alisema mtaalamu huyo.

Alisema   utafiti huo   unaendelea kufanyika katika hatua nyingine   kuona jinsi ya kukabiliana na panya waliopo   mashambani.

“Mlipuko wa panya ni mkubwa  na kama tusipopata njia za kuwadhibiti, hali katika mashamba yetu inaweza kuwa mbaya kabisa,” alisema.

ONDOA NYWELE USONI KWA KUTUMIA BINZALI



Yes ladies kila mmoja wetu anavinyweleo usoni, but sema tu kwa wengine huonekana more kuliko wengine..na kama bado hujapata solution ya kuondoa basi leo ndio nimewaletea..Nadhani utakuwa umenotice kuwa ukipaka makeup au hata powder tu inakuwa inakaa kwa juu ya vinyweleo na huleta muonekano mbaya, basi fuata hii process fupi tu kuweza kuondoa vinyweleo usoni.

1. Chukua vijiko 2 vikubwa vya binzari manjano, changanya na maji ya uvuguvugu kidogo upate mchanganyiko mzito.


2. Paka katika sehemu ambayo unataka vinyweleo hivyo kuondoka kabisa, then acha ikae kwa dakika 20-30.


3. Chukua kitambaa na maji ya baridi kisha lowesha kitambaa na uanza kusugua hiyo sehemu uliyopaka mchanganyiko wako wa binzari manjano.


Fanya hivi kila siku, na siku sinavyozidi kwenda utaona vinyweleo vinapungua na hatimaye kuisha kabisa. Hii itafanya iwe vigumu kwa vinyweleo kuota usoni.

Alhamisi, 21 Julai 2016

NIMEPATA FAIDA NYINGI TANGU NIACHANE NA MAGROUP YA WHATSAPP



Habarini ndugu!
nina siku nne nimeachana na matumizi ya smartphone(hasa magroup ya whatsap yasiyo natija),al-mahsusi hizi app za whatsapp na instagram.nataka niwashirikishe watanzania wenzangu uzoefu wangu huu wa miezi miwili, nadhani inaweza kuwasaidia baadhi ya watu!

Pamoja na faida chache au nyingi za mitandao hii,nilikuja kugundua hizi app hasa whatsapp ilikuwa inanipotezea sana muda na kuniharibia concentration kwenye mambo ya msingi zaidi katika utafutaji hivyo kupunguza uzalishaji, na kupunguza kasi ya kufikiri!

Baada ya kuachana na matumizi haya ya whatsapp/smartphone nimejikuta nimekuwa effective sana kwenye kazi zangu kwa maana ya kuutumia vizuri muda wangu,napata muda wa kutosha kusoma vitabu,kufikiri,ku meditate,kuandika vitabu nk,


Stress zimepungua,nimefakiwa kupunguza stress za aina mbalimbali ambazo zinasabishwa na chatting nyingi zisizo za msingi au picha na video za ajabuajabu,zimebaki stress za kusaka hela tu..

Mahusiano yameimarika;mahusino na watu wangu hayajatetereka tena, kwa sababu hatuwasiliani mara kwa mara hivyo hakuna makwazo yanayotokana na kuwasiliana mara kwa mara
Akiri imekuwa focused zaidi na kazi:Concentration kwenye kazi imeongezeka sana na kuondoa blockage za sms za whatsapp zinazoingia masaa 24..
hizo ni baadhi tu, kuna nayaona matokeo makubwa zaidi baadae..

HOFU YANGU,
Tunatengeneza taifa la mashabiki na watu wasioweza kufikiri tukiendekeza hili, watu wanachati tu hata wakiwa maofisini, tena wanachat umbeaumbea tu,mpira,ajali,picha za uchi,kudharauriana kwenye magroup na kutukananank
taifa linaangamia,nani atalizuia au kulisemea hili, ni kitu chenye impact kubwa sana in the long run.

taifa linaongeza watu wavivu,watu wenye tabia mbovu,wambea,walalamikaji nk.. where are we heading as a nation?

tutegemee thinkers wachache sana baadae

najua wale addicts watapinga sana hili, lakini huu ndo ukweli mchungu

tafari..chukua hatua

KINANA ANENA,ALIMKATALIA JK BAADHI YA MAMBO



KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ametoa neno endapo Rais John Magufuli atamhitaji kuendelea na wadhifa huo, huku akibainisha kuwa amekutana na changamoto nyingi katika nafasi hiyo kiasi kwamba wakati mwingine alikata tamaa.

Mwanasiasa huyo maarufu ndani ya CCM na nchini, anatarajiwa kuhitimisha uongozi wake wiki hii wakati Mwenyekiti mpya wa CCM Taifa, Rais John Magufuli atakapokabidhiwa uenyekiti huo na kuunda Sekretarieti yake mpya ambayo haijulikani kama itaongozwa tena na Kanali huyo wa zamani wa Jeshi.

Akizungumza jana na waandishi wa habari baada ya kukagua Ukumbi wa Mkutano Maalumu wa CCM utakaofanyika keshokutwa Jumamosi, Kinana ambaye amekuwa katika nafasi hiyo kwa miaka mitatu na nusu, alisema aliombwa katika nafasi hiyo baada ya kuwa aliamua kustaafu, lakini akakumbana na changamoto mbalimbali.

CCM kuwa mbali na wananchi Alisema kuna wakati aliona kama vile chama kiliacha kwenda kwa wananchi na kwamba hakikuwa karibu sana nao.

“Ninyi ni mashahidi, ikabidi kubuni utaratibu mzuri wa kwenda kwa wananchi ili chama kiwe karibu na wananchi, kiwasikilize na kuwa sauti ya wananchi kifuatilie matatizo yao kisimamie utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi,” alisema Kinana na kuongeza kuwa katika kufanya hivyo amekuwa akiwasiliana na Rais na Waziri Mkuu kwa ajili ya matatizo kutatuliwa.

“Changamoto ya pili ya kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya chama, hapo nyuma kulikuwa na misukosuko kidogo ya umoja na mshikamano, kushutumiana na kulaumiana,” alisema na kuongeza kuwa kazi nyingine aliyofanya ni kuimarisha umoja ndani ya chama, kushirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha chama kinajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kurejea katika misingi yake ya awali katika maeneo ya uadilifu, uwajibikaji na utendaji kazi kwa ufanisi.

Azuiwa ziarani

Kinana alisema amekwenda wilaya zote, majimbo, mikoa na nusu ya kata za nchi na amesafiri zaidi ya kilometa 192,000, kufanya mikutano zaidi ya 3,700 ya aina mbalimbali ya ndani na nje na haikuwa kazi rahisi “Changamoto nilizokutana nazo ambazo lazima nikiri ni pale nilipotaka wakati mwingine kufanya ziara kwenye maeneo fulani fulani niliambiwa ni hatarishi siwezi kwenda kwa hiyo ilibidi nibishane na viongozi na watendaji wakuu wa serikali…nikasema hapana nimeamua kwenda lazima niende,” alisema Kinana.

Katibu huyo akitoa mfano alisema kuna wakati aliamua kutoka kwa boti kutoka Nyamisati wilayani Rufiji kwenda Mafia, viongozi wa Mkoa wa Pwani walifikiri si njia salama ya kusafiri na kumpelekea ujumbe asisafiri kwa boti, bali asafiri kwa ndege, lakini alisema hapana ataondoka kwa boti.

“Walichofanya wakakaa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wakaniandikia barua rasmi kwamba tunakushauri usisafiri kwa boti safiri kwa ndege kwa maana nyingine walikuwa wanajivua lawama kwa yatakayotokea, lakini vile vile kunitisha kidogo kwamba si salama zaidi nikawasisitiza hapana,” alieleza Kinana.

Ashitakiwa kwa JK

“Baadaye Rais mstaafu Kikwete alikuwa Msoga, viongozi wa Mkoa wa Pwani wakaenda kumwambia tumezungumza na Katibu Mkuu wako naona hasikii tumemuandikia barua ya kumuomba asisafiri na boti hasikii, Rais akaandika meseji ndefu sana…nikamjibu rais nakuheshimu mamlaka yako ni makubwa si vizuri nikakukatalia, lakini niruhusu nikukatalie kwa sababu hata wananchi wanaosafiri kwenye boti hii wanahatarisha maisha yao, ni vizuri na mimi nikahatarisha maisha yangu hata kidogo… akaniambia nimekuelewa endelea,” alibainisha.

Alisema zipo changamoto nyingi sana nyingine, kwa mfano Mbambabay kwenda Kyela, mkuu wa mkoa akamuambia boti haifai kusafiri akasema mara haiwezi kusafiri imeharibika.

“Nikazungumza na Mwakyembe akapeleka mafundi wakatengeneza, safari haikuwa rahisi, lakini changamoto zilikuwa nyingi sana, kwingine Lupingu kule ni gari moja tu ndio inayoshuka chini hakuna kupishana magari nikaambiwa nisiende nikasema nina kwenda,” alisema na kuongeza kuwa kulikuwa na ubishi mwingi wakati mwingine alionekana mtu mmoja kidogo ambaye hasikilizi ushauri sana.

Pia nyingine zinazotokana na changamoto za wananchi kutolipwa mazao yao kwa wakati, mbolea kutofika kwa wakati, halmashauri kutopata fedha za maendeleo kwa wakati, watumishi wa umma wanaohamishwa kwenda vijijini hawaendi vijijini kwenda kuwahudumia wananchi, tatizo kubwa la migogoro kati ya wakulima na wafugaji kati ya wananchi na hifadhi za taifa.

“Ndio maana mnaniona siku hizi nimenyamaza kwa sababu yale yote niliyokuwa nikiyaombea yanafanyika, umangimeza haupo watu wachape kazi wawahudumie wananchi, uadilifu unapigwa vita, rushwa inapigwa vita, uwajibikaji na uadilifu unahimizwa, utendaji kazi unatakiwa na hayo yasipofanyika mtu anaondolewa mara moja,” alifafanua Kinana ambaye kuanzia mwaka 2014 hadi mwanzoni mwa mwaka jana alitembea kote nchini akikisafisha chama chake na kuibana serikali.

Kurejea kwake CCM

“Yalitokea mazingira ambayo niliombwa na viongozi wastaafu na viongozi wa chama kuniomba niwe mtendaji mkuu wa chama chetu. Si nafasi ambayo niliipenda, bali niliitwa na nikakalishwa wakanisihi na mimi nikakubali sababu ni wito na kwa kuwa ni watu ninaowaheshimu na wana dhamana kubwa kwenye nchi yetu, nikakubali kufanya kazi hiyo,” alisema Kinana akizungumzia jinsi alivyoteuliwa kushika nafasi hiyo.

Alisema amekuwepo katika uongozi ndani ya chama kwa muda mrefu (miaka 25) ndani ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, na alihisi ni wakati muafaka wa kung’atuka.

“Mwanasiasa mzuri ni yule anayejua wakati wa kuingia na wakati wa kutoka. Ni wakati mzuri wa kung’atuka kuachia waingie wenye umri wa kati na umri wa vijana kuachia waongoze chama na kuwaamini,” alieleza.

Alisema moja ya mambo ambayo walikubaliana wakati ule akajitahidi kukiimarisha chama, kusimamia na kumsaidia mwenyekiti kusimamia mchakato wa kuwapata wagombea kwenye nafasi zote za Urais, Ubunge na Udiwani. Pia alijitahidi kuendesha shughuli za kampeni na uchaguzi na utakamalizika.

“Uchaguzi umekwisha niruhusiwe kupumzika, na wote waliafiki na kukubali sasa muda umefika kwa hiyo nimewakumbusha yale tuliyokubaliana muda wake umefika sasa wengine wakaniuliza hivi ndivyo tulivyokubaliana nikawaambia wazee hamjawa wazee kiasi cha kusahau ndio haya tuliyokubaliana,” alieleza.

Akiombwa na JPM

Alipoulizwa kama akiombwa na Rais Magufuli aendelee kwa Katibu Mkuu, Kinana alisema, “Niseme hajasema, hatujazungumza hilo, likitokea tutaangalia, tutakaa naye kikao kama akiniomba, tutakuwa na kikao na mazungumzo muda utakapofika kama nilivyokuwa na mazungumzo na kikao kama kwa wale walioniomba mwaka 2012.”

Waliokisaliti chama

Akizungumzia walioisaliti CCM katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, mtendaji huyo wa CCM alisema msaliti yeyote adhabu yake ni mbaya sana, hata kwenye chama cha siasa.

“Kwenye CCM wapo watu walioyumba, kulikuwa na wimbi kubwa mwaka jana, watu waliyumba hivi kidogo wakakaa mguu upande huku hawapo na kule hawapo, wako ambao sio tu waliyumba, bali walikiuka maadili na hawakushiriki kwenye shughuli za kampeni,” alisema.

Pia alisema wapo ambao hawakushiriki, hawakusaidia na wakasaidia upinzani na kila mtu atakuwa na adhabu yake kulingana na makosa yake.

“Kama mmekuwa mkifuatilia kuna waliochukuliwa hatua ngazi za wilaya na mikoa. Kwa mfano, Shinyanga 123 walichukuliwa hatua. Wapo wanaotakiwa kuchukuliwa hatua kwenye ngazi za juu, sasa jambo moja mtu yeyote kabla ya kuchukuliwa hatua lazima aelezwe mashtaka yake, apewe fursa ya kusikilizwa, kwa hiyo hawa wote watasomewa mashtaka, watasikiliza na kupewa adhabu kwa kadri itakavyostahili, lakini hatua zitachukuliwa mara baada ya Mkutano Mkuu kumalizika,” alieleza.

LOWASA: MAGUFULI AMEBAGUA



ALIYEKUWA mgombea urais kupitia mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amewataka vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumlinda Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kama nyuki wanavyomlinda malkia wao.

Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alitoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha Kamati ya Utendaji ya Baraza la Vijana (Bavicha) jijini Dar es Salaam jana.

Waziri mkuu huyo wa zamani, pamoja na mambo mengine aliwataka vijana wa chama hicho kuacha vita vya ndani kwa ndani na badala yake washikamane na kuwang’ang’ania viongozi wanaowaongoza.

“Tuache vita vya ndani kwa ndani, Mbowe ndiye mwenyekiti wetu wa chama…tumlinde kama nyuki wanavyomlinda malkia wao. Mtu akishakuwa kiongozi tumg’ang’anie,”alisema Lowassa.

Lowassa ambaye alijiunga na upinzani mwishoni mwa mwaka jana alisema kumekuwapo na kawaida ya kuibuka kwa makundi uchaguzi unapomalizika.

Azungumzia uchumi
Katika mkutano huo, Lowassa pia alizungumzia uchumi ambapo alisema hivi sasa maisha ya Watanzania walio wengi hayana uhakika, huku matumaini kidogo yakielekezwa kwa watu wachache.

“Binadamu anaishi kwa matumaini, lakini mambo yanayoendelea hapa nchini hayatoi matumaini hayo…hali ya uchumi inakwenda vibaya sana, kuna rafiki yangu mmoja ana msamiati wake anasema maisha ni pasua kichwa hivi sasa kwa sababu hayana uhakika,” alisema Lowassa.

Aidha Lowassa alieleza kusikitishwa kwake kwa baadhi ya watu kuacha kuzikana kwa sababu ya siasa ambapo alisema hayo ni mambo ya ovyo.

Ajivunia vijana
Katika hotuba yake hiyo, Lowassa aliwapongeza Bavicha kwa kutii maelekezo ya Mbowe kuhusu kusitisha uamuzi wao wa kwenda Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Niwapongeze kwa kutii maelekezo ya mwenyekiti wetu, najua haikuwa rahisi, mlikuwa mmeshajipanga lakini maelekezo ya mwenyekiti ni mazuri, vitu vingine si lazima uende mbali sana ni kama kwenye simu kwamba ‘message sent’ mlifikisha ujumbe mahsusi hata kama hawakubaliani lakini ujumbe umefika.

“Wala msione aibu mnachofanya, vijana mngefanya tofauti ningeshangaa, nyie ndio chachu ya mabadiliko lazima mje na kitu kipya na mawazo mapya, ninyi ni jeshi la chama.

“Kwa uzoefu wangu CCM lazima watakwenda kumtambulisha mwenyekiti wao mpya katika Uwanja wa  Jamhuri mjini Dodoma, hivyo wananchi wenyewe wataangalia na kupima kama Chadema wanazuiwa kwa nini wapinzani wazuiwe, waachane wapate tabu kujieleza kwa umma” alisema Lowassa huku akishangiliwa.

Kuhusu uteuzi uliofanywa na Rais John Magufuli hivi karibuni, Lowassa aliuponda na kusema ni wa kibaguzi kwa sababu umewatenga vijana wa vyama vya upinzani.

“Kama wewe ni CCM utakuwa mkuu wa wilaya, mkoa na hata mkurugenzi wa halmashauri lakini hali ni tofauti kwa vijana wa upinzani, wanabaguliwa utadhani si Watanzania.

“Hili ni jambo la kutafakari na kukemea kwa sabu ajira ni tatizo hapa nchini, lakini hata hizo chache zinatoka kwa kubaguana pamoja na jitihada zote lakini hazisaidii,”alisema.

YANGA WAINGIA KAMBINI




Kikosi cha Yanga SC kinatarajiwa kuingia kambini leo kuanza rasmi maandalizi ya mchezo wa marudiano wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Medeama FC ya Ghana.

Yanga watakuwa wageni wa Medeama Jumatano ya Julai 27, mwaka huu Uwanja wa Sekondi Sports au Essipong mjini Sekondi-Takoradi, Ghana katika mchezo huo wa kwanza wa marudiano mzunguko wa pili Kombe la Shirikisho, siku ambayo vinara wa kundi hilo, TP Mazembe wataikaribisha Mouloudia Olympique Bejaia mjini Lubumbashi.

Timu hizo zitarudiana kiasi cha wiki baada ya kutoa sare katika mechi zao za kwanza, Yanga ilikubali sare ya 1-1 na Medema huku MO Bejaia ikitoshana nguvu ya sare ya 0-0 na Mazembe.