Jumatatu, 18 Julai 2016
UVCCM YAWASAKA VIJANA WA CHADEMA (BAVICHA),DODOMA
KAIMU Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka amewasili mkoani Dodoma na kuhoji waliko vijana wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) waliotangaza kutaka kuuvuruga Mkutano Mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii.
Shaka alisema yuko mkoani hapa kwa ajili ya kuongoza harakati za kukilinda chama hicho kwa kushirikiana na vijana wa CCM.
Alisema UVCCM imeandaa vijana 30,000 maalumu kwa ajili ya kulinda mkutano huo utakaohudhuriwa na viongozi wote wa juu wa serikali na CCM.
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema aliwasili mapema mkoani Dodoma ili pamoja na mambo mengine ashuhudie vurugu zilizoahidiwa na Bavicha lakini, hadi sasa hakuna chochote.
“Nipo hapa kwa muda mrefu kwa ajili ya kuongoza shughuli za ulinzi wa chama na viongozi wetu nikiwa mtendaji mkuu na mtoa maelelezo ya kiitifaki.
“Kwa bahati mbaya kwa muda wote huo sijaona dalili wala hata harufu ya Bavicha. Hii inadhihirisha kwamba kusema na kutenda ni vitu tofauti,”alisema Shaka.
Alisema azma ya UVCCM ilikuwa ni kuithibitishia dunia kwamba Watanznia hawako tayari kuona kundi lolote la wahuni likichafua amani, utulivu na usalama wa watu na likaachwa litambe bila kufundishwa.
Shaka alisema, wajumbe wa mkutano huo hawapaswi kuwa na hofu juu ya usalama wao na mali zao na kuwaomba waingie Dodoma wakiwa na imani na watatoka salama kwa kuwa vijana wa kuwalinda wapo wa kutosha.
PICHA:JINSI ZITO ZUBERI KABWE ALIVYOUAGA UKAPELA
Pichani ni Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe ameuacha rasmi ukapera baada ya kufunga ndoa na Mpenzi wake aliyemvisha pete ya uchumba miezi miwili iliyopita, ndoa na tafrija zote zimefanyika Zanzibar
July 14, 2016.
Jumapili, 17 Julai 2016
TCU YATOA SIFA MPYA ZA KUJIUNGA NA VYUO
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza utaratibu mpya kwa watahiniwa wa mwaka mpya wa masomo wa 2016/2017 wanaochukua shahada, huku wanafunzi wengi wakiwa hatarini kukosa nafasi kwa kukosa sifa na vigezo.
Utaratibu huo mpya umekuja ikiwa ni miezi miwili sasa tangu kutumbuliwa kwa watendaji wa tume hiyo kutokana na kudahili wanafunzi wasio na sifa na kusababisha kupewa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Sifa hizo ziliwekwa mapema wiki hii katika tovuti ya TCU na kurudiwa jana. Taarifa hiyo inaonyesha kutolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wa tume hiyo, Eliuta Mwageni.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa njia ya simu jana, Ofisa Habari Mwandamizi wa TCU, Edward Mkaku, alithibitisha taarifa ya utaratibu huo mpya.
Mkaku alisema utaratibu huo umetolewa baada ya mwaka jana kutumika mfumo wa wastani wa pointi (GPA) ambao Januari, mwaka huu, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, aliagiza ufutwe na kurudishwa ule wa madaraja (division) uliotumika siku zote.
“Mfumo wa udahili uliotumika mwaka jana ulikuwa ni GPA na mwaka huu utatumika mfumo wa divisheni, ndiyo maana utaratibu huo ukawekwa,” alisema Mkaku.
Moja ya sifa zinazotakiwa katika udahili wa mwaka huu wa masomo (2016/2017), ni wahitimu wa kidato cha sita waliomaliza kabla ya mwaka 2014 kuwa na ufaulu wa (D mbili) pointi 4.0.
Mchanganuo ulionyesha kuwa pointi hizo zinatokana na ufaulu wa A = 5; B= 4; C= 3; D = 2; E = 1.
Taarifa hiyo ilionyesha kuwa ili wahitimu wa kidato cha sita kwa mwaka 2014 na 2015 wawe na sifa za kudahiliwa, watatakiwa kuwa na alama za ufaulu wa (C mbili ) pointi 4.0 kupitia mchanganuo wa A = 5; B+ = 4; B = 3; C= 2; D = 1.
Pia tovuti hiyo ilionyesha kuwa wahitimu waliomaliza kidato cha sita kwa mwaka huu, watahitajika kuwa na ufaulu wa alama (D mbili) 4.0 kupitia mchanganuo wa A = 5; B = 4; C= 3; D= 2; E = 1.
Mbali na sifa hizo, watakaodahiliwa ni wale ambao pia watakuwa na utambulisho wa sifa za kielimu za kidato cha nne ambazo ni kuanzia alama nne za D na kupanda juu katika mchanganuo wa alama za ufaulu wa B+, ikiwa A =75-100, B+ = 65-74, B=50-64, C=40-49, D=35-39, F= 0-38.
Sifa nyingine zinazotakiwa ni wenye cheti cha NVA daraja la tatu pamoja na ufaulu wa si chini ya alama nne za D za kidato cha nne au sifa nyingine zinazokaribiana na hizo, ikiwa ni pamoja na zinazotambuliwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) au Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Pia watahiniwa hao watatakiwa kuwa na angalau GPA ya 3.5 kwa stashahada (NTA) daraja la sita au wastani wa B kwa cheti cha ufundi (FTC) katika mchanganuo wa alama A=5, B=4, C=3 na D=2 au wastani wa daraja la B+ kwa wenye stashahada za ualimu, au wastani wa daraja la B+ kwa kitengo cha afya kama tabibu wa magonjwa ya binadamu na nyingine au cheti na stashahada nyinginezo.
Sifa nyingine zinazoangaliwa katika udahili huo ni kuwa na ufaulu wa daraja la pili kwa wenye stashahada zisizokuwa za NTA.
Pamoja na hayo, TCU ilisema hakutakuwa na usajili wa mafunzo ya awali pamoja na yale ya UQF6 yaliyozuiwa kuanzia mwaka wa masomo wa 2016/2017.
Taarifa ya tovuti hiyo iliendelea kusema kuwa maombi yote ya usajili wa wanafunzi hao wanaotaka kuchukua shahada yanatakiwa kupitia TCU pekee.
“Kwamba tume hiyo imeamua kuwa kuanzia mwaka 2016/2017, maombi yote ya usajili kwa makundi yote yanayoanzia aya ya 3.0 kwenda juu wataunganishwa na TCU pekee na walio chini ya hapo hawatahusika na tume hiyo,” ilisema taarifa hiyo.
Pia TCU ilisema taarifa hiyoni kwa mujibu wa kipengele cha 5(1)(c)(i) cha katiba ya vyuo vikuu, kifungu cha 346 cha sheria nchini.
“Msingi wa kubadili viwango vya kujiunga na elimu ya juu ni kutokana na kuwepo maoni kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya uwezo wa wahitimu wanaojiunga na vyuo vikuu mbalimbali,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mei, mwaka huu, Profesa Ndalichako aliwasimamisha kazi Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya, kwa kushindwa kuisimamia tume hiyo kutokana na kuwapo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa, kisha wakadahiliwa katika vyuo vikuu na kupata mkopo.
Wengine aliowasimamisha kazi ni Mkurugenzi wa Ithibati na Udhibiti Ubora, Dk. Savinus Maronga, Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Rose Kiishweko na Ofi sa Msimamizi Mkuu wa Taarifa, Kimboka Stambuli.
Pia Mei mwaka huu, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idrisa Kikula, alitangaza kuwasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 7,000 wa kozi maalumu ya stashahada ya ualimu ambao hawakuwa na sifa.
Alipozungumzia sakata hilo Juni, mwaka huu wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais Dk. John Magufuli, aliwaita wanafunzi hao kuwa ni vilaza, na kwamba idadi kubwa ya waliofukuzwa hawakuwa na sifa stahiki za kudahiliwa kusoma kozi hiyo.
FILAMU YA AISHA YASHINDA TUZO
Filamu ya Aisha iliyotayarishwa na Chande Othman imefanikiwa kushinda tuzo nne usiku kupitia tuzo ya mtayarishaji bora Bongo Movie, Mwigizaji bora wa kike ni Godliver Gordian aliyeigiza kama Aisha, Best Feature Film ni Godliver Gordian na mwongozaji bora ni Amil Shivji kupitia filamu ya Aisha.
Jumamosi, 16 Julai 2016
MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA NDOA
Ndoa ni makubaliano ya watu wawili kati ya mwanamke na mwanaume ambao wako tayari kuacha familia zao na kuanzisha yao kama wandani kwa kushirikiana katika mambo yote kwa shida na raha hadi kifo kinapo watenganisha.
Furaha ya ndoa ni kumpata yule umpendaye na ambaye ni chaguo la moyo wako na tulizo la mwili wako lakini pia furaha ya ndoa ni kufuatisha mambo 6 ya muhimu zaidi yatakayo zidisha furaha hiyo ndani ya nyumba yako.
MAWASILIANO.
Kuwa tayari muda wote kumsikiliza mwenzako, Baada ya ratiba ngumu za siku kuwa na hamu ya kumsikiliza mwenzako kwa kumuuliza maswali mbalimbali, lakini kumbuka wakati mwingine hata mke au mume wako naye anahitaji kukuuliza au kukusikiliza, hivyo epuka sana kutoa hitimisho wewe tu, fungua masikio yako na msikilize kile anachosema mwenzako.
UPENDO.
Unaweza kuwa mbali na mume au mke wako lakini unaweza kumudu kuongea na umpendaye hata kwa njia ya simu, ili mradi tu onesha kuwa unampenda na kumjali.
Onesha unampenda saana mke au mume wako daima. Kila siku hakikisha unadhihirisha upendo wako kwake usichoke.
Mbusu mke au mume wako, mkumbatie kila mara kama ishara ya upendo,Kama mtapendana kwa dhati basi bila shaka mtaheshimiana, na kila mmoja atamthamini mwenzake,kila siku tafakari kwa nini ulimpenda yeye tu na wala si mwingine, hii itakufanya umpende zaidi mke au mume wako.
MVUMILIE
Wanandoa wanaofanikiwa kuishi muda mrefu wakiwa na furaha daima ni wale wanaovumilia hali zote za maisha; Mfano; wakati wa magonjwa, wakati wa utajiri, wakati wa umaskini, wakati wa afya njema.
Kama wanandoa wataweza kuvumiliana katika hali zote hizi basi wataishi kwa furaha kwa sababu watakuwa wamezipitia nyakati zote hizi, hivyo kila mmoja ata muona mwenzake ni muhimu zaidi.
MUWAZIE MEMA MWENZA WAKO.
Ndoa nyingi zimekuwa zikifurahia maisha ya ndoa kwa sababu wote wanawaziana mema. Mhurumie umpendaye, mjali mtie nguvu pale ambapo anakata tamaa, weka upendo wako wote kwake.
SAMEHE NA JUA KUSAHAU.
Wana ndoa wanaofanikiwa katika maisha yao ya ndoa ni wale wanao pokea na kutoa msamaha.
Ni wale wanao samehe na kusahau kabisa makosa ya wapenzi wao akati wanapofanya makosa ambayo yanawaumiza wapenzi wao wana omba msamaha.
MTHAMINI MKE AU MUME WAKO.
Ili kila mmoja awe na amani katika ndoa ni lazima kila mmoja awe na mchango sawa katika mahusiano usioneshe kuwa wewe ni bora kuliko mwenzi wako hii ita mfanya mwenzako ajisikie hana uhuru ita hafifisha mahusiano yenu kama mke au mume.
BODI YA MIKOPO YAPEWA MASAA 72
Kamati ya mawaziri wa mikopo ya serikali za wanafunzi wa Elimu ya juu nchini Tanzania inayoundwa na mawaziri, Manaibu waziri na makatibu wa wizara ya mikopo kutoka vyuo vyote nchini leo July 16 2016 wamkutana na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa kamati Taifa, Shitindi Venance amesema kipindi cha mwisho wa mwezi huu wanafunzi wa elimu ya juu watatakiwa kufika katika vituo vyao vya kazi vilivyosambaa nchi nzima ili kuendelea kupata mafunzo kwa vitendo ila wamesikitishwa kwamba wakati wakijiandaa na hilo hakuna mchakato wowote unaoendelea kupelekea kupata fedha hizo, Shitindi amesema…….
>>>Mpaka sasa hivi tukiwa tumebakiwa na takribani siku tano kabla ya kufunga chuo hakuna hata karatasi za kusaini zilizotumwa vyuoni ili kukamilisha zoezi hilo na mchakato wa kusaini hukuchukua muda wa siku tatu mpaka tano
>>>Kutokana na ucheleweshaji huo tunatoa muda wa saa 72 kuanzia leo Jumamosi, mpaka Jumanne ya wiki ijayo kwa bodi ya mikopo kufikisha fedha za kujikimu wakati wa mafunzo kwa vitendo katika vyuo vyote hapa nchini ili wanafunzi waweze kusaini na kupokea malipo yao:-Shitindi
MEYA DAR AMFUNDA MAKONDA
Yafuatayo Ni muhimu Kwa wakaaz wa Jiji la Dar kufahamu kama haki yao ya msingi kabla ya utekelezwaji wa amri ya Mh Mkuu wa mkoa wa Dar wa kufanya msako kwenye makazi na nyumba zao.
Moja: Kwanza zoezi hili ni BATILI na haliwezi kutekelezeka kwenye Halmashauri zetu za Jiji la Dar es Salaam
Pili: Nawaomba sasa nielezee sababu ambazo nasema agizo hilo na zoezi hilo litakuwa BATILI :
A. Sheria ya makosa ya Jinai Inaelezea utaratibu wa kukaguliwa nyumbani kama search warrant ambayo inatolewa Na Mahakama au polisi, Na ambayo Inaelezea wanatafuta nini
B. Sheria hiyo pia inamtaka mwananchi kuwakagua maafisa wa Mahakama Na Polisi watakaofika Nyumbani kwake ili wasiweze kumpandikishia ushahidi wa uongo
C. Kamwe popote duniani Kibali cha wananchi kukaguliwa majumbani hakiwezi kutolewa Na Viongozi wa kisiasa.
D. Kwa maagizo hayo inasemekana wananchi watawekwa ndani Kwa kukataa kutii agizo hilo, hakuna sheria Tanzania inayoruhusu Mwananchi kuwekwa ndani kwa sababu za hovyo Kama hizo.
Naomba nimalizie Kwa kusema wananchi wote wa Jiji la Dar wawe na Amani kabisa na wajue haki zao na wajue kuzitetea, sisi viongozi wao tupo imara kusimamia haki zao na maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.
Issaya Mwita Charles
Mstahiki Meya Jiji la Dar es Salaam
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)