Jumapili, 11 Septemba 2016
HIZI NDIO MBINU ZA KUMNASA MTEJA KWENYE BIASHARA YAKO
Kazi kubwa sana unayohitaji kufanya baada ya kumpata mteja ni kuhakikisha anaendelea kuwa wako, yaani anaendelea kufanya biashara na wewe.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kuwafikisha wateja kwenye biashara zao, lakini wateja wanapofika na kupata huduma huondoka na wengi kutokurudi tena.
Ni rahisi sana kumuuzia mteja ambaye ulishamuuzia awali, kuliko kumuuzia mteja mpya. Hivyo kama ukiweza kuiendesha biashara yako vizuri, wateja ambao wananunua kwako watakuwa wateja wako wa kudumu.
NAPENDA BIASHARA
Zifuatazo ni mbinu kumi unazotakiwa kuanza kuzitumia leo kwenye biashara yako ili kuhakikisha wateja wako wanaendelea kufanya biashara na wewe.
1. Tekeleza ulichoahidi.
Kama umemtangazia mteja kwamba akija kwenye biashara yako atapata kitu fulani, basi hakikisha anapata kitu hiko. Hakuna kitu ambacho watu hawapendi kama kudanganywa. Mteja anapoona kwamba amedanganywa hatorudi tena kwenye biashara yako na utakuwa umemkosa milele. Hakikisha unatimiza ulichomwahidi mteja wako.
2. Ahidi kikubwa na pitiliza(overpromise and overdeliver)
Najua hapa unaweza usielewe kwa sababu ulichozoea ni kuahidi kidogo na kupitiliza(underpromise and overdeliver). Hii ilikuwa unafanya kazi zamani, ila kwa sasa, haifanyi kazi tena. Kwa sababu kama wewe unaahidi kidogo, wenzako wanaahidi kikubwa na wanafanyia kazi. Hivyo kitu pekee cha kuhakikisha unawabakisha wateja ni kuwaahidi makubwa na kuyapitiliza hayo. Kama umejitoa kweli kwenye biashara yako, hili halitakushinda.
3. Imarisha mawasiliano yako na wateja wako.
Ni muhimu sana uwe na mawasiliano na wateja wako. Bila ya kujali ni biashara gani unafanya, kuna na mfumo w akupata namba za simu, au barua pepe za wateja wako. Mata kwa mara watumie ujumbe ukiwatakia heri na wakati mwingine kuwajulisha bidhaa au huduma mpya zilizopo kwenye biashara yako.
4. Fanyia kazi malalamiko ya wateja haraka.
Wateja wanapokuwa na malalamiko, yafanyie kazi haraka sana. Usisubiri mpaka yawe makubwa kiasi cha kuwafanya watafute mahali pengine wanakoweza kufanya biashara bila ya matatizo wanayopata kwako.
5. Toa huduma bora ambazo mteja hawezi kupata popote.
Huduma kwa wateja, mteja amepokelewaje, ameelezwaje kuhusiana na bidhaa au huduma anayohitaji, maswali yake yamejibiwaje, hivi ni vitu vinavyoonekana vidogo sana ila vina maana kubwa sana kwa wateja wa biashara yako. hakikisha wateja wako wanapata huduma ambazo zitawafanya wajisikie ufahari.
6. Wakumbuke wateja waliopotea.
Kama biashara yako imekuwepo kwa muda, kuna wateja waliokuwepo awali ila kwa sasa hawapo tena. Kuna wateja ulikuwa unafanya nao biashara zamani, ila kwa sasa huwaoni tena kwenye biashara yako. ni vyema kuwatafuta na kujua kwa sasa biashara wanafanya na nani na ni kitu gani limewafanya hawaji tena kwako.
7. Muuzie mteja baada ya kumuuzia.
Mara nyingi mteja atakuja kwako akitaka kitu fulani, lakini pia anaweza kuwa anataka vingine zaidi ya alichofuata hapo. Ni jukumu lako kujua mahitaji haya yote ya mteja wako na kuyafanyia kazi. Usiishie kumuuzia mteja kitu kimoja pekee, hakikisha kila anachohitaji ambacho kipo kwenye biashara yako, unampatia. Ataendelea kuja kwako kwa sababu anajua mahitaji yake yote anayapata kwako.
8. Pima thamani ya mteja ya muda mrefu.
Kuna wateja ambao wananunua mara moja na kuondoka na kuna wateja ambao wataendelea kununua kwako kwa muda mrefu. Wateja wanaonunua mara moja na kuondoka unaweza kupata faida kubwa, lakini ndio imeishia hapo. Wateja ambao wananunua muda mrefu unaweza kupata faida ndogo, ila utaendelea kuipata kwa muda mrefu. Jua wateja wale wa muda mrefu na endelea kuwapatia thamani nzuri.
9. Tumia mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii kuwa karibu na wateja wako.
Mtandao umerahisisha sana mfanyabiashara kuwa karibu na wateja. Hakikisha biashara yako ipo kwenye mtandao kwa kuwa na tovuti, kuwa na blogu na kuwa na kurasa kwenye mitandao ya kijamii. Utatumia mitandao hii kutoa taarifa muhimu kuhusiana na biashara yako.
10. Toa zawadi na motisha kwa wateja.
Kuwa na njia ambapo utatoa zawadi mbalimbali kwa wateja wanaorudi tena kwenye biashara yako. inaweza kuwa kuwapatia kuponi za punguzo kadiri wanavyonunua mara nyingi, au kutoa punguzo la bei kama mteja ananunua mara nyingi. Vyovyote vile hakikisha mteja anapata motisha pale anaponunua kwako kwa muda mrefu.
Anza kufanyia kazi mambo hayo kumi ili kuboresha uhusiano wako na wateja wako na uweze kukuza biashara yako.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni