Alhamisi, 28 Septemba 2017

KABLA YA KUANZA BIASHARA/KAZI MPYA FANYA HAYA KWANZA


"Hodi Hodi.....!" Ilikuwa ni sauti ya kijana Mike ambaye sikumtia machoni miaka mitatu iliyopita.
"Karibu sana Kijana Habari za siku nyingi"Ilikua ni sauti ya Bundala Izengo Mwandishi wa Makala haya baada ya kutembelewa na kijana Mike ofsini kwake.

Sura ya Mike ilionekana yenye huzuni,aibu hata asili yake ya kujiamini ilipotea,mikunjo ya ngozi yake na mapere katika paji la uso(chunisi) na ngozi iliyofubaa na kupoteza rangi yake ya asili vilinisababisha kutoa chozi la huruma kwa kijana huyu ambaye alikuwa ni jirani yangu pia rafiki yangu kibiashara.

Si kwa sababu ya maradhi la hasha,hii ni kwa sababu ya maisha magumu aliyonayo baada ya kuacha biashara aliyokuwa anaifanya na iliyokuwa ikimuingizia faida nono baada ya kuambiwa na ndugu zake kuwa kuna biashara ambayo ingemwingizia kipato kedekede,Sio dhambi wala kosa kuacha biashara uliyonayo bali ni kosa kubwa kuacha biashara inayokuingizia kipato bila kufuata taratibu zifuatazo.

1.FANYA UTAFITI WA KUTOSHA
Ni dhahiri kuwa Mike hakuzingatia kipengele hiki muhimu cha uanzishaji wa biashara,hata kama alikifanya basi ni kwa kiwango cha chini kabisa,kipengele hiki kinakusanya mambo mengi ikiwemo kuandaa Mpango wa biashara, ni vyema zaidi ukawashirikisha wataalamu wa mahesabu ya biashara ambao watakusaidia mambo mengi ya kufanya kabla na baada ya kuanza biashara.

2. ZUNGUMZA NA WABOBEVU KATIKA BIASHARA HIYO
Hii ni hatua muhimu kabla ya kuanza kufanya biashara mpya waulize wenyeji wa biashara hiyo mambo mbalimbali yanayohusu biashara unayotaka kuifanya,ikiwezekana omba kazi mahali hapo hata kwa kujitolea ili uweze kujua changamoto za kazi hiyo japokuwa changamoto zingine hauwezi kuzijua mpaka utakapoingia rasmi kwenye biashara hiyo. Wakati hayo yote ukiyafanya usisahau kufanya hili lifuatalo ambalo Mike hakulifanya.

3. USIFUNGE BIASHARA YA MWANZO.
Ghafla Mike alipotea machoni pangu,duka lake akalifunga akawa anakuja kuchukua baadhi ya vitu na kuviuza kwa watu tena kwa bei ya hasara,nilijaribu kumuuliza ni kitu gani kimemkuta aliniambia maneno haya

"Huku mambo yametiki babu njoo tujichanganye kwenye biashara ya kuleta mazao ya viazi Mbatata jijini Dar es salaam" Sikukomea hapo nilijaribu kumshauri neno hili

"Mwachie mdogo wako au ajiri mtu aweze kukuendeshea biashara hii,huko uliko unawezakukwama ukarudi kwenye biashara yako ya awali."Mike alinitiazama kisha akacheka na kuniambia.

"Hapana Bundala,nafanya hivi ili kuongeza mtaji wangu kwani kiasi nilichonacho hakitoshi"Sikuchoka kumuuliza maswali ili niweze kujua faida inayopatikana katika biashara yake mpya,lakini nilipomujliza swali hili ndipo nikaumia zaidi
"Mtaji uliutoa wapi kijana mpaka ukaweza kufanya mambo makubwa kama haya?" Baada ya kunijibu swali langu hili,ndipo nilishangaa na kustaajabu ya Musa na baada ya miaka mitatu niliyaona ya Filauni, Majibu ya swali langu yalikuwa hivi.

4.USIKOPE ILI KUANZISHA BIASHARA MPYA
Watu wengi hufurahia kupata mkopo kwa sababu ni pesa ambayo unaipata bila ya wewe kuteseka wakati wa kuitafuta,sasa jua ya kuwa baada ya kukopa utateseka kuitafuta kwa ajili ya kurudisha mkopo.Kama tayari ulishaanza biashara yako na unataka kubadili biashara ni bora ukaweka akiba yako mpaka itakapojitosheleza.
Majibu ya swali langu yalikuwa ni hivi

"Nilikopa kwenye benki moja,kulingana na dhamana niliyonayo Walikubali kunipatia Milioni 10 hivyo ndio maana nimeanzisha niashara hivyo basi kutokana na ukubwa wa mtaji huo sioni sababua ya kuendelea kufanya biashara hii ya zamani"Alizungumza Mike na kuondoka.Niliwaza juu ya maisha aliyonayo wakati huo,niligundua ya kuwa, kwa mtaji huo Mike atakua ametusua (kufanikiwa).

5. HAKIKISHA UNA AKIBA YA KUTOSHA
Mwalimu wangu wa Ujasiliamali na Uwekezaji Dr. Amani Makrita,aliwahi kunifundisha somo hili ambalo ni muhimu sana endapo utadhamiria kuanza kufanya biashara mpya.Baada ya kupata mafunzo haya nilimkumbuka Kijana Mike Ambaye hakuweza kufuata kanuni hii pengine kwa kujua au kutokujua.Dr. Amani alisema hivi

Unapotaka kubadili biashara,hakikisha umeweka akiba ya kutosha katika akaunti yako,Hakikisha una pesa ya kuweza kuhudumia familia yako kuanzia chakula,malazi,mavazi na kulipia karo za shule kwa muda wa miezi sita ijayo,hakikisha una pesa ya kutosha ya kulipia madeni ya mikopo ya benki/binafsi kwa muda wa miezi sita bila kutegemea pato la biashara yako Mpya,uwe na akiba ya Nusu mtaji wako mpya kwa ajili ya kukabiliana na majanga au hasara.

Hili ndio lilikuwa kosa kubwa alilolifanya Mike ambaye aliingia katika biashara mpya akiwa na mkopo benki,bila ya kuweka akiba ya miezi sita ijayo.Baada ya kufanya biashara kwa muda wa miezi miwili Mike alipata ajari ya gari na kupoteza mali zake zote.
Maisha yaligeuka,alikimbilia kusikojulikana na kuacha mali zake Nyumba,kiwanja alizoweka dhamana zikachukuliwa na benki,Maisha yalikuwa magumu mpaka siku ha kwanza aliporudi mjini, nilijifunza mengi juu ya mkasa huu.
Nina imani unayesoma makala Haya hautaweza kufanya makosa kama ya Mike Jipange katika mambo hayo niliyokuorodheshea pindi unapotaka kufanya biashara Mpya au Kuacha kazi na kufanya kazi/biashara nyingine.

Hadithi hii ni ya kutunga haina ukweli wowote juu ya Maudhui na Majina. Mtindo uliotumika ni mtindo wa Darasa kwa njia ya hadithi.
Asanteni sana ni mimi BUNDALA ABELY IZENGO 0656669989

Jumatano, 6 Septemba 2017

MAMBO YANAYOSABABISHA MATUMIZI MABAYA YA PESA.


Kila kukicha matumizi ya pesa yanazidi kuongezeka hali ambayo inasababisha pesa iwe na majina mengi kama faranga,mshiko,mapene,ndarama,fulusi,senti,mbago,shekeli n.k.Kubadilika kwa majina haya si kwa bahati mbaya bali ni kwa sababu watu wanaipenda pesa na wanaitafuta pesa kila kukicha.

Unaweza kukubali kuwa kuitafuta pesa ni jambo moja na kuitumia pesa ni jambo jingine.Je ni wangapi wanaoitafuta pesa usiku na mchana wakiipata wanakwenda kuweka heshima baa?Je ni wangapi wanaotafuta pesa kwa jasho jekundu lakini matumizi yao yanaishia kwa madada poa?

Leo katika somo letu kwa njia ya hadidhi tutajifunza juu ya MAMBO AMBAYO YANASABABISHA MATUMIZI MABAYA YA PESA.
Katika familia tunazoishi matumizi mabaya ya pesa hurudisha nyuma maendeleo ya familia nilifanikiwa kusikiliza mzozo huu wa wanandoa hawa.

1. MATUMIZI YASIYO YA LAZIMA
"Hodi ndani" Ilikuwa sauti ya Bundala mwandishi wa makala haya alipomtembelea rafiki yake Shafii nyumbani kwake.
"Karibu baba mdogo"Sauti ya Jane (mtoto wa kwanza wa Shafii ilisikika ikinikaribisha) Niliingia ndani na kuketi juu ya kiti.
Ghafla nilisikia minong'ono iliyoashiria kuna shari chumbani kwa Shafii.

"Wewe unatumia vibaya pesa juzi umenunua Dela, Jana gauni leo unataka pesa kwa ajili ya kiatu wakati nguo na viatu unavyo tele!"Hii ilikuwa ni sauti ya rafiki yangu Shafii ambaye alikuwa akimgombeza mkewe kwa kumtuhumu kuwa anatumia vibaya pesa.

Uwepo wangu mahali pale nilihisi wa bahati mbaya,niliweweseka kimawazo na kushindwa kufanya uamuzi wa haraka,nilimtizama mtoto Jane alishindwa kuniangalia,mzozo uliendelea sasa haikuwa siri tena kwani sauti zilisikika kwa kila aliyekuwa karibu.

"Wewe kila siku unapanda boda boda ukitaka kwenda kazini na ukiwa unarudi mbona mimi sikuambii,unatumia shilingi elfu nne kila siku kwa ajili ya bodaboda ilhali ungeweza kutembea kwa miguu mpaka nyumbani si ungeweza kuokoa Laki moja na elfu ishirini (120,000/=) kwa mwezi?"Alihoji mkewe Shafii.

Umbali wa kutoka nyumbani mpaka barabarani ni mita mia mbili sawa na urefu wa viwanja viwili vya mpira.
Niliwaza juu ya hoja zao mbili ambazo zinaonekana dhahiri kuwa ni wivu wa matumizi mabaya ya pesa, nilipata jibu kuwa wote wana matumizi yasiyo ya lazima.

2: KUIGA TABIA ZISIZO NA MATOKEO MAZURI

Watu wengi hufanya kwa sababu wamemuona mtu flani anafanya,hivyo hupelekea kuishi maisha ya kuigiza kila siku,maisha haya hayana faida yeyote.Huwezi jua kwa nini yule anafanya hivyo yawezekana akawa na sababu ambazo wewe huzijui.

Mkasa wa Shafii na Mkewe uliendelea huku maskio yangu yakisikiliza kwa makini
"Nilishakuambia hao marafiki zako wanaokufundisha huu ujinga wa kuhudhuria kila harusi ya hapa mtaani sitaki kuwaona tena hapa nyumbani"Shafii alizungumza kwa hasira.

"Siwezi kuwaacha marafiki zangu nitaendelea kuwa nao na nitahudhuria sherehe kila napopata mwaliko,pesa ni ya kwangu,mshahara ni wangu halafu wewe unanipangia magumizi thubutuu"Ilikuwa ni sauti ya mke wa shafii ilisikika na kukatishwa ghafla.

"Hodi baba,baba mdogo amekuja" Jane alikuwa akimwita baba yake .

"Mkaribishe ndani"Baba yake alimjibu.

"Yupo amekaa kwenye kochi"Jane alimjibu baba yake huku akiusukuma mlango na kuingia chumbani kwa baba yake.

Shafii alitoka chumbani kwake na kuja sebureni,Sura yake ilijawa na aibu kiasi kwamba hata kunisalimu alipatwa na kigugumizi.

Nilimchangamkia ili niweze kundoa aibu aliyokuwanayo na niliyokuwanayo, Baada ya dakika tano kupita Shemeji(mkewe shafii) alikuja sebleni akiwa amefura na kifua kikiwa kimejaa hasira,hapo ndipo mambo yakawa hivi.(soma namba 4).

Ili uweze kufanikiwa ni lazima uachane na marafiki walio na fikra hasi juu ya maisha,wanaowaza kitchen party,vigodoro na mizimbao,walio na matumizi mabaya ya pesa,jiangalie wewe ulipo na unapokwenda kwani hakuna anayeweza kuubeba mzigo wako vijana wa siku hizi wanasema PAMBANA NA HALI YAKO.

4.KUTOKUWA NA BAJETI.

Bajeti ni muongozo wa matumizi ya pesa ambayo inakuwa imeandikwa katika karatasi,vifaa vya electronics n.k.Bila ya kuwa na bajeti kusingekuwa na mpangilio mzuri wa matumizi ya serikali,makampuni hata mtu binafsi.

Tunaendeshwa na bajeti ili kuweza kufikia malengo yetu tuliyojiwekea,kutokuwa na bajeti hatuwezi kufanya chochote wala malengo hatutayafikia.

Tukiwa tumekaa sebuleni walinieleza sababu ya ugomvi wao ambazo zililemea kwenye matumizi mabaya ya pesa katika mambo ambayo hayana umuhimu wala faida katika maisha yao.

Suala la bajeti ya pesa walizokuwa wanazikusanya lilikuwa ni shubiri kwao,kupelekea matumizi mabaya ya pesa na mara nyingine kukosa pesa ya chakula nyumbani na kusababisha madeni mengi na makubwa dukani kwa Mangi.

5. HISIA ZA KUPATA TENA KESHO

Hili ni suala ambalo watu wengi linawaathiri na athari zake zinakuja kuonekana hapo baadae,msemo wa tumia pesa ikuzoee umekuwa ni miongoni mwa misemo ambayo inaleta matokeo hasi katika maisha ya vijana wengi.

"Kwani shemeji nikipata mshahara wangu wa laki 5 kwa mwezi nikatumia laki 3 kwa ajili ya kununua nguo na mambo mengine,nikaweka laki 2 ya chakula nyumbani kuna ubaya gani?"Ilikuwa sauti ya Mke wa shafii ambaye alitaka ufafanuzi.
Swali hili limejengwa katika misingi ya "kesho nitapata hata kama nikitumia vibaya siku ya leo"Kitu ambacho ni sumu katika ustawi wa uchumi wa familia yako.

Pia maisha ya hawa wawili hayakuwa na mikakati kuhusu miaka 10 ijayo,bajeti zao zilikomea mwezi mmoja tena za kununua nguo za harusi.Maisha haya hautakiwi kuishi wewe unayesoma makala haya,Ishi maisha ya bajeti yenye matumizi mazuri ya pesa hapo ndipo utafikia uhuru kifedha.
Hadithi hii ni ya Kubuni haina ukweli wowote na majina yaliyotumika
Tembelea Blog Hii ya patamamboadress.blogspot.com

Mwandishi wa makala haya Bundala Izengo.0656669989


Jumatatu, 4 Septemba 2017

JE.NI SAHIHI KUCHAGULIWA KAZI/BIASAHARA YA KUFANYA?


Hili ni swali lililokosa majibu ya haraka baada ya kuulizwa na mdogo wangu ambae yuko chuo kikuu mwaka wa tatu hapa nchini Tanzania.
Nilihisi kama utani kumbe alikuwa akimaanisha na akitaka jibu sahihi na lenye muongozo katika hitaji lake la kujikimu kimaisha.
Swali hili lilinifanya nichakate akili na kujaribu kumweleza A na B nyeusi na nyeupe juu ya harakati za kutafuta maisha hasa kwake yeye ambaye bado ni mwanachuo.

Kijana huyu alikuwa na Wazo lake la biashara ambalo hakika analipenda na aliamini kuwa lingeweza kumfikisha kileleni kifedha na kujaribu kukidhi mahitaji yake muhimu.Kwa kuwa kijana huyu alikuwa bado yuko mikononi mwa wazazi ilimlazimu kuwashirikisha wazazi wazo lake,hapo ndipo alipokutana na vigingi.

"Baba nahitaji kufungua banda kwa ajili ya kuonyesha mpira"Ilikuwa ni sauti ya kijana huyu ambayo ilikuwa ikiomba ruhusa.
"Sawa lakini subiri kwanza tujadili na mama yako"Baba alimjibu huku akishangazwa na wazo la mwanae.
Saa zilipita na siku zikasogea bila ya kupata jibu la ombi lake.Aliamua kujaribu kumweleza mama yake

"Mama nina wazo la biashara ya kuonesha mpira kwani maeneo haya hakuna huduma hiyo hivyo vijana huenda kusini na mahariki ya jirani kutafuta huduma hiyo hasa wakati wa msimu wa mipira ya ulaya,ligi kuu Tanzania kombe la Afrika na dunia."Kijana huyu alizungumza na mama yake akimuomba apate ruhusa hiyo.

"Tumejadili na baba yako tumeona kuwa kuonyesha mpira unaweza kukusababishia kuharibika kimaadili kwa sababu wateja wako watavuta sigara,bangi,pombe na wengine kugombana hata kutukanana pia imani yetu hairuhusu ushabiki wa mpira,hivyo tumejadili na kuona kuwa sio vyema kukuruhusu kufanya biashara hiyo ambayo inamchukiza Mungu ni vyema uanzishe biashara ya kuchoma mahindi!"Alizungumza mama yake akisahau ya kuwa kijana wake ni shabiki damudamu wa Klabu ya mpira ya Man United na Simba.

"Daaahh sawa mama nimewasikia wazazi wangu"Ilikuwa ni ya sauti ya chini na huzuni ya kijana huyu ambaye ndoto zake ziliyeyuka mithiri ya barafu kwenye jua.

JE WAZAZI WALIKUWA SAHIHI KUMCHAGULIA KIJANA WAO KAZI BIASHARA?

Katika misingi ya mafanikio moja ya msingi wa mafanikio ni kufanya ukipendacho matharani hakivunji sheria za nchi,hicho ndicho kitakufikisha katika kilele kifedha,kulingana na jibu la wazazi wake alikata tamaa katika harakati zake za kutafuta maisha hivyo aliamua kunifuata kuniomba ushauri,kwani wazo la wazazi wake ilikuwa ni vigumu kulivuata kwa sababu hajawahi kulifanyia utafiti na wala hajawahi kufikilia kama siku moja atafanya biashara hiyo.

Sikuwa na hiana nilijaribu kumweleza mambo ambayo yanaweza kusababisha mtu kuchagua kazi.

1.SHERIA ZA NCHI
Kila nchi imetunga sheria zake kulingana na uhitaji wa sheria hizo kwa wanachi wake,mara nyingi sheria za nchi huwa hazibagui dini kabila wala utaifa Mfano.Ukibainika kuwa una kosa wewe ni mgeni katika nchi flani utahukumiwa kulingana na sheria za nchi hiyo.Hivyo basi ni vyema unapochagua wazo lako la biashara lisije likawa kinyume na sheria za nchi hiyo.Mfano Kenya ni ruhusa kutumia mirungi kwa ajili ya tiba,Tanzania ni kosa kubwa kutumia mirungi haijalishi kwa ajili ya tiba au biashara.Hivyo basi ukiangalia sheria za nchi hizi mbili zinakinzana ukitaka kufanya biashara hiyo ni bora ukahamia huko.

2.DINI
Hili ni tattizo kubwa sababu, dini zimekuwa zikichanganya waumini wake na kila kiongozi amekuwa akitafasiri mambo kulingana na yeye alivyoelewa,huwa nafikia wakati nasema ukisikiliza sana unaweza kuchanganyikiwa ukashindwa kufanya jambo lolote.Hawa wanasema Soda ni mbaya na hairuhusiwi kutumika kwa kinywaji, wengine wanaenda mbali zaidi wakipiga marufuku waumini wao kutumia baadhi ya vinywaji baridi wakifananisha majina ya vinywaji hivyo na madawa ya kilevya n.k
Ukweli ni kwamba miruzi hii inatupoteza mwelekeo, Mdogo wangu nakusihi fanya kile ukipendacho bila kuvunja sheria za nchi na maandiko ya Mungu wala sio fikra za watu.

3.MILA NA DESTUTI
Japokuwa sababu hizi zinaweza kuwa sababu za kizamani lakini bado kuna watu wanaendekeza Mila na Destuli katika kufanya kazi.Mila zimekuwa mwiba kwetu kwa sababu watu wamekuwa wakibagua kazi wakisema.
"Kazi hii ni ya mwanaume, na ile ni ya kike"Hizi ni sauti za watu ambao ni maskini wa mawazo,katika ulimwengu huu wa sayansi na technolojia uliochagizwa na ugumu wa maisha hakuna ubaguzi wa kazi wa namna hiyo Japokuwa bado watu wanafikra hizo.Miaka ya 199 - 2011 ilikuwa ni vigumu kukutana na konda mwanamke/Rubani wa ndege mwanamke lakini sasa hivi ni kawaida kuwaona akina dada wakichangamkia fulsa japokuwa jamii inaweza kukuchukulia katika mtizamo Chanya au Hasi.

4.MAZINGIRA.
Mazingira yanayotuzunguka yanaweza yakawa ni sababu ya kuchagua kazi,lakini pia mazingira haya haya yanawezakuwa fulsa kwetu hauwezi kufanya biashara ya kuuza barafu katika maeneo ya baridi kali hata kama unapenda biashara hiyo,lakini katika mazingira haya biashara ya kuuza kahawa na chai inalipa na chenji inabaki.

"Sawa kaka nimekuelewa"sauti ya mdogo wangu ilinifanya nikomee hapo na kuendelea kupiga soga nyingine zikiwa ni pamoja na kukagua mpango wake wa biashara ya kuonyesha mpira.Navyozungumza hiii leo amekuwa ni tegemezi nyumbani kwao.
Nimeandika haya ili nikutie moyo kijana mwenzagu usisikilize kelele za watu mbalimbali(akili za kuambiwa hanganya na zako),siku zote wanaoharibu mipango yako ni watu wa karibu yako.FANYA BIASHARA UIPENDAYO BILA KUVUNJA SHERIA ZA NCHI.

Nawatakia kazi njema Ni mimi Bundala .A. Izengo